Waislamu, Wakristo Burkina Faso Wala Futari Pamoja

Mamia ya Waislamu na Wakristo huko Ouagadougou, mji mkuu wa Burkina Faso, wameshiriki pamoja dhifa ya futari katika medani ya Place De La Nation, kuadhimisha mwaka wa tatu wa utamaduni huo wa kuhamasisha mshikamano wa kijamii, wakati huu ambapo nchi hiyo inakabiliwa na ghasia za itikadi kali.

Hafla hiyo imeandaliwa na chama cha vijana kinachohamasisha watu kuishi kwa umoja licha ya tofauti za kidini na kutoa kipaumbele kwa mazungumzo na diplomasia.

Viongozi wa kidini na kijamii waliozungumza kwenye hafla hiyo wamesisitizia haja watu wa dini tofauti kuvumiliana na kuishi pamoja kwa amani.
Moumini Koudougou, mratibu mkuu wa shughuli hiyo amesema, “Burkina Faso ni familia moja. Huu ni wakati wa kusherehekea umoja wetu, haswa wakati wa Ramadhani na Kwaresima.”

Naye Malik Ouédraogo, muumini wa Kiislamu aliyeshiriki dhifa hiyo ya futari jana amesema: Mpango huu unaimarisha udugu na mshikamano wetu, ukiondoa vikwazo vinavyoweza kutugawa.”

Kwa upande wake, Wendnonga François Sawadogo, Mkristo Mkatoliki aliyeshiriki futari hiyo ya pamoja anasema, “Ninatumaini kwamba mwaka ujao, amani itakuwepo, ili tuweze kusherehekea kuishi pamoja tukiwa ndugu wa dini zote.”

Burkina Faso imekabiliwa na mwongo mmoja wa ukosefu wa usalama kutokana na makundi ya kigaidi yenye mafungamano na Al-Qaeda na Daesh (ISIS); magenge ambayo yanayochochea mivutano baina ya jamii.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii