Rwanda imetangaza Jumatatu, Machi 17, kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Ubelgiji, ikishutumu serikali ya zamani ya kikoloni kwa "kuunga mkono" Kinshasa "kabla na wakati wa mzozo unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)."
"Serikali ya Rwanda leo imeijulisha Serikali ya Ubelgiji kuhusu uamuzi wake wa kuvunja uhusiano wa kidiplomasia, mara moja," Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda imesema katika taarifa yake. Uamuzi unaohusishwa, kulingana na Kigali, na "majaribio ya kusikitisha" ya Brussels "kudumisha dhana zake za ukoloni mamboleo."
Ubelgiji "inasiitishwa" na uamuzi "usio na uwiano" wa Rwanda wa kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na itatangaza wanadiplomasia wa Rwanda walioko kwenye ardhi yake kuwa watu wasiostahili, amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Maxime Prévot.
"Leo, Ubelgiji imeonyesha wazi kuengemea upande mmoja katika mzozo wa kikanda na inaendelea kuhamasisha kwa utaratibu dhidi ya Rwanda katika majukwaa mbalimbali, kwa kutumia uongo na ghiliba ili kujenga maoni ya chuki isiyo na msingi dhidi ya Rwanda, kwa lengo la kuvuruga nchi na kanda nzima," Kigali imeshutumu. “Uamuzi wa leo unaonyesha dhamira ya Rwanda katika kulinda maslahi yake ya kitaifa na utu wa Wanyarwanda, pamoja na kuzingatia kanuni za kujitawala, amani na kuheshimiana,” imeongeza taarifa hiyo. Wanadiplomasia wote wa Ubelgiji waliopo nchini Rwanda wanatakiwa kuondoka nchini Rwada ndani ya saa 48, Kigali imesema.
Ubelgiji, nchi ambayo ni mkoloni wa zamani wa DRC (zamani Zaire) na Rwanda, imekuwa moja ya nchi muhimu zaidi kwa ukosoaji wake dhidi ya Kigali tangu waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Kigali walipoanzisha mashambulizi mashariki mwa DRC mwezi Desemba, ambapo walichukuwa udhibiti wa Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, na Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini.
Hasa, Brussels iliutaka Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi wa Januari kuzingatia vikwazo dhidi ya Rwanda, inayoshutumiwa kwa kukiuka mamlaka ya DRC. Ubelgiji haikuunga mkono kifurushi kipya cha msaada cha euro milioni 20 kilichotolewa mnamo mwezi wa Novemba. Ilijizuia kupiga kura katikakikao cha Baraza la EU.