Bunge la Seneti kujadili hoja ya kumuondoa madarakani naibu wa rais Rigathi Gachagua

Bunge la Seneti limekutana katika kiako cha dharura kupokea hoja kutoka kwa Kiongozi wa walio wengi Aaron Cheruyot baada ya Baraza la Wawakilishi kupiga kura ya kumuondoa madarakani Gachagua siku ya Jumanne Oktoba 8, 2024.

Bunge la Seneti nchini Kenya litaanza kujadili hoja ya kumuondoa madarakani Naibu wa rais Rigathi Gachagua siku za Jumatano na Alhamisi wiki ijayo siku moja baada ya Baraza la Wawakilishi kupiga kura ya kumuondoa madarakani.

Bunge zima la Seneti litachunguza mashtaka dhidi ya Gachagua na kusikiliza ushahidi kutoka pande zote .

Wabunge 281 nchini Kenya waliunga mkono hoja ya kumuondoa madarakani naibu wa rais Rigathi Gachagua siku ya Jumanne. Kiwango kilichowekwa na katiba ni angalau wabunge 233.

Kiongozi huyo alikabiliwa na makosa 11 ya ufisadi, kutumia vibaya madaraka na kukiuka katiba. Hii ni mara ya kwanza kwa naibu wa rais kuondolewa madarakani kwa njia hii chini ya katiba mpya ya 2010.

Hoja ya kumwondoa Gachagua madarakani iliwasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse. Itakumbukwa kuwa wabunge walianzisha mchakato wa kumtimua Gachagua Oktoba mosi mwezi huu pale 291 walipotia saini hoja ya kumtimua.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii