BODI ya Wakurugenzi ya Taasisi ya
Mwalimu Nyerere (MNF), inayomaliza muda wake imemteua Joseph Butiku kuwa
mwenyekiti mpya wa bodi hiyo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mwenyekiti
wa bodi aliyemaliza muda wake, Jaji mstaafu Joseph Warioba wakati
akiitambulisha bodi mpya ambayo itakuwa na wajumbe 10.
Warioba
amesema bodi iliyomaliza muda wake ambayo ilikuwa inaongozwa na Balozi
Dk.Salim Ahmed Salim imefanikiwa kwa kiasi chake hivyo wanaamini kuwa
bodi mpya itaendeleza mazuri waliyofanya.
Amesema Hayati Mwalimu
Julius Nyerere alianzisha taasisi hiyo mwaka 1996 ikiwa haina fedha ila
walijitahidi kusuluhisha migogoro ya ndani na nje ambapo moja ya
mgogoro waliofanikiwa ni wa Burundi.
Ameongeza wamekuwa
wakipitia changamoto mbalimbali ila wanashukuru wameweza kuzivuka."Tangu
mwaka 1996 tumekuwa tukishiriki kwenye mazungumzo ya maridhiano ambapo
mengi ya mazungumzo yameweza kufanikiwa ni imani yetu kuwa bodi mpya
ambayo ina wajumbe wa zamani wawili itaendeleza utaratibu huo kwa
maslahi ya Tanzania na Afrika kwa ujumla."
Warioba ametoa rai kwa
Watanzania kuiunga mkono bodi hiyo mpya ili iweze kutimiza malengo hayo
ambayo mwasisi wake Hayati Nyerere aliyasisi.
Kaimu Mwenyekiti
huyo, alitaja wajumbe wapya wa bodi ni Profesa Tarsis Kabwegijere,
Balozi Amina Salum Ally, Neema Nyerere, Geoffrey Israel, Catherine
Mgenda, John Kyaruzi, Balozi Celestine Liundi, Profesa Penina Mlama na
Profesa Martha Koro.
Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa
mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Butiku alisema mipango yake ni kuhakikisha
dhana ya amani, umoja na maendeleo kwa kasi ambayo italeta mabadiliko
chanya kwa wananchi na nchi
Butiku ambaye pia ni Mkurugenzi
Mtendaji wa MNF amesema katika uongozi wake atahakikisha kasi ya
kudumisha umoja, mshikamano na maendeleo inafanikiwa.
"Mimi nipo
kwenye hii taasisi tangu 1996 malengo na matarajio yake nayajua na
nimekuwa nikiyatekeleza naamini nafasi hii itanipa nguvu zaidi kusukuma
mbele zaidi," amesema.
Butiku amesema taasisi hiyo itahakikisha
malalamiko yote ya kisiasa, kijamii, uchumi na maendeleo yanapata
muafaka kwa njia shirikishi kwani ndio lengo la Hayati Nyerere.