Gari la uchukuzi wa umma limekumbwa na shambulizi la bomu kaskazini mwa Kenya, karibu na mpaka wa Somalia.
Waandishi wa habari wa eneo hilo wanasema takriban watu tisa wamefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa. Gari hilo lilikuwa likisafiri kuelekea Mandera, mji ulio katika eneo la mpakani, ambao umekuwa ukiathiriwa mara kwa mara na mashambulizi ya wanamgambo.
Picha kutoka kwa wanahabari wa eneo hilo zinazoshirikishwa katika mitandao ya kijamii zinaonesha mabaki ya gari la umma, linalojulikana kama matatu, ambalo lilipuliwa baada ya kukanyaga kilipuzi kilichokuwa kimetegwa barabarani.
Hakuna aliyedai kuhusika, lakini waasi wa Al Shabaab wamekuwa wakiwalenga polisi na raia ndani na karibu na Mandera na vifo kadhaa katika miaka ya hivi karibuni, na kuifanya Mandera kuwa moja ya maeneo hatari zaidi ya Kenya kuishi.
Shambulio hilo limetokea wiki moja tu baada ya balozi kadhaa za kigeni nchini Kenya, zikiwemo Marekani na Ufaransa, kuwaonya raia wake kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi nchini humo.
Polisi wa Kenya wametoa taarifa kuwahakikishia wananchi usalama wao.