WAKALA wa Barabara nchini (Tanroads)
imepiga hatua nyingine, baada ya kukamilisha ujenzi wa daraja la urefu
wa mita 98 katika mto Ruhuhu linalounganisha wilaya ya Nyasa mkoa wa
Ruvuma na Ludewa mkoa wa Njombe .
Baadhi ya wahandisi wa
Tanroads kutoka mikoa mbalimbali nchini walioshiriki kujenga daraja hilo
walisema, kukamilika kwa daraja hilo ambalo limejengwa kwa ubora wa
hali ya juu na wahandisi wa Kitanzania ni mafanikio makubwa kwa Serikali
ya awamu ya sita.
Mhandisi Mwandamizi wa Tanroads Makao makuu
Secilia Kalangi alisema, daraja la Ruhuhu limejengwa kwa vyuma badala ya
zege na wataalam wa Kitanzania kutoka mikoa 26 ya Tanzania kwa
kushirikiana na wataalam wa Tanroads makao makuu.
Kalangi
alisema, daraja limekamilika kwa asilimia mia moja na ameipongeza
wakala wa Barabara nchini( Tanroads) kuwaamini waandisi wake ambao
walifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha ujenzi wa mradi huo muhimu
kwa uchumi unakamilika kwa wakati.
Kalangi ambaye alikuwa
kiongozi wa Timu ya waandisi hao, ameishukuru Wizara ya Ujenzi kuwapa
dhamana ya kutekeleza mradi huo mkubwa ambao ulikuwa unasubiriwa kwa
hamu na wananchi wa mikoa hiyo miwili.
Alisema, hatua ya
serikali kuwatumia wahandisi wa ndani imesaidia kuokoa fedha nyingi kama
ingewatumia wakandarasi wa nje,pia daraja hilo limetumika kama sehemu
ya mafunzo kazini kwa waandisi wazalendo katika kujenga madaraja ya
aina hiyo ambayo ni machache hapa nchini.
Aidha alisema, sehemu
hiyo ilikuwa shida kupitika kutokana na kuwepo kwa wanyama wakali hasa
mamba na viboko ambao walitishia na kupoteza maisha ya wananchi wengi
walipotaka kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
Ndiyo
maana,serikali iliamua kujenga daraja kutokana na changamoto ya usafiri
kati ya mkoa ya Ruvuma na Njombe na baada ya kukamilika limerudisha
matumaini kwa wananchi wa mikoa hiyo ambao wameanza kufurahia matunda ya
Serikali yao.
Mhandisi Vicent Shirima kutoka Tanroads mkoa wa
Njombe, alitaja fursa zinazoweza kupatikana baada ya kukamilika kwa
daraja ni pamoja na kusafirisha makaa ya mawe yanayochimbwa kwa wingi
wilaya ya Ludewa kwenda Bandari ya Mtwara .
Shirima alitaja
manufaa mengine ni kuwawezesha wakulima,wafanyabiashara na wananchi
kusafirisha mazao na bidhaa zao kwenda katika mikoa mbalimbali nchini
kutafuta masoko na amewataka kutumia daraja hilo kuongeza uzalishaji na
kufanya biashara,badala ya kuacha fursa hiyo ikiwanufaisha watu kutoka
nje ya mkoa huo.
Naye Mkuu wa kitengo cha mipango Tanroads mkoa
wa Ruvuma Msama Msama alisema,daraja hilo linatimiza adhima ya Tanroads
kuunganisha watu wa sehemu moja na nyingine, kukuza uchumi na
kuharakisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Nchi kwa ujumla.
Alisema,daraja la Ruhuhu limejengwa katika nguzo kuu nne zilizobebwa na
msingi wenye nguzo nyingine ndogo(Piles)48 na umegharimu jumla ya
Sh.8,976,808,037.64.
Kwa mujibu wa Msama, baada ya kukamilika
kwa ujenzi huo kilichobaki ni wananchi wenyewe kutumia fursa hiyo
kusafirisha bidhaa kwani limekuwa mkombozi mkubwa kwao.
Amewataka,wananchi wanaoishi vijiji jirani vya Lituhi kwa upande wa
Nyasa na Kipingu Ludewa kulinda daraja hilo kwa kuwa ni mkombozi mkubwa
kwao, hivyo lazima walilinde kwa gharama yoyote ili liwasaidie katika
shughuli mbalimbali za kiuchumi na kutambua kuwa Serikali imetumia fedha
nyingi.
Kwa upande wake Mhandisi Geroge Nyagaboma kutoka
Kilimanjaro alisema,watatumia ujenzi wa daraja la Mto Ruhuhu kama sehemu
ya mafunzo kazini kwa kujenga madaraja mengine hapa nchini kwa weledi
mkubwa.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kipingu kata ya Manda wilayani
Ludewa Elasmus Mbeya,amefurahishwa na hatua ya Serikali kukamilisha
mradi huo ambao umerahisisha mawasiliano kati ya mkoa wa Njombe na
Ruvuma ambayo inategemeana katika mambo mbalimbali ya kiuchumi na
kijamii.
Daraja la Mto Ruhuhu linalounganisha wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma na Ludewa mkoa wa Njombe lililojengwa na Wahandisi wa Tanroads kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara kama linavyoonekana baada ya kukamilika rasmi ambapo limeanza kutumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa hiyo miwili.
.Baadhi ya Wahandisi kutoka Wakala wa Barabara nchini(Tanroads) Secilia Kalangi,George Nyagaboma na Msama Msama wakiangalia sehemu ya daraja la mto Ruhuhu linalounganisha mikoa ya Njombe na Ruvuma baada ya kumaliza kazi ya ujenzi wa Daraja hilo ambalo limegharimu zaidi ya Sh.bilioni 8.
Waandishi walioshiriki kujenga daraja la Mto Ruhuhu linalounganisha mikoa ya Njombe na Ruvuma, kutoka kushoto Vicent Shirima wa Tanroads mkoa wa Njombe,Mhandisi Mwandamizi Secilia Kalangi wa Makao makuu ya Tanroads,Msama Msama kutoka mkoa wa Ruvuma,na Geroge Nyagaboma kutoka mkoa wa Kilimanjaro na Afisa Uhusiano wa Tanroads Lela Haji wakitembea juu ya daraja hilo baada ya kukamilika rasmi ujenzi wake na kuanza kutumika.
Kivuko cha Mv Ruhuhu kilichokuwa kikifanya kazi ya kusafirisha watu na
mizigo katika Mto Ruhuhu kikiwa kimepaki baada ya kukamilika kwa Ujenzi
wa Daraja katika mto huo.