Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amekutana na balozi wa Misri nchini Tanzania
Mhe. balozi Mohamed Gaber Abulwafa na kujadiliana masuala mbalimbali ya
Uwekezaji na fursa mbalimbali zilizopo baina ya nchi hizi mbili.
Mhe.
Dkt. Kijaji amesema kuwa uhusiano na ushirikiano wa Uwekezaji baina ya
Misri na Tanzania umekuwa ukiimarika zaidi baada ya ziara ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya
tarehe 10 Novemba, 2021 kukutana na Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah Al
Sisi.
Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa fursa za biashara na
uwekezaji kati ya Misri na Tanzania ambapo kwa hivi sasa biashara baina
ya nchi hizo mbili imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 84.3 mwaka 2018
hadi kufikia Shilingi Bilioni 87.3 mwaka 2020 hivyo kuna kila sababu
yakuendeleza majadiliano na makongamano ya biashara baina ya nchi hizi
mbili ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara kutumia fursa za uwekezaji.
Naye
balozi wa Misri nchini Tanzania Mhe. Balozi Mohamed Gaber Abulwafa
amesema kuwa Nchi ya Misri imewekeza nchini Tanzania katika miradi 26
yenye thamani ya kiasi cha Shilingi Trilioni 3.1 na kutengeneza ajira
2,206 kwa watanzania.
Mhe. Balozi Mohamed Gaber Abulwafa amesema
kuwa wawekezaji kutoka Misri walishafika nchini Tanzania katika
Kongamano la Biashara lililofanyika nchini Tanzania ambapo
wafanyabiashara wa Misri walipata fursa mbalimbali za kuwekeza na sasa
wanaendelea na taratibu mbalimbali kuja kuwekeza Tanzania katika sekta
ya Kilimo na Mifugo hasa biashara ya korosho, parachichi na Mahindi.
Aidha
ameongeza kuwa Misri wapo katika hatua za ukamilishwaji wa kuanza kwa
usafiri wa abiria kwa njia maji marine transport kutoka Misri hadi
Tanzania ili kukuza Uwekzaji na Biashara na kurahisha usafirisjhaji wa
bidhaa katika nchi hizi mbili.
Mhe. Dkt. Kijaji amemalizia kwa
kusema kuwa Nchi ya Misri imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya
kimkakati katika nchi ya Tanzania ukiwemo ujenzi wa mradi wa Bwawa la
Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP-MW2115) unaotarajiwa
kukamilika Mwezi Juni 2022 na kusaidia Viwanda vyetu kuzalisha kwa
uhakika kwani changamoto ya umeme nchini itakuwa imekwisha.