WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mhandisi Hamad Masauni, amelitaka Shirikika la Umoja wa Mataifa la
Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini kufanya kazi kwa kuzingatia sera,
sheria na vipaumbele vya Serikali katika utendaji wake.
Masauni
amezungumza hayo jijini Dar es Salaam,katika Kikao na Mwakilishi Mkazi
mpya wa Shirikika hilo Nchini, Mahoua Bamba Parums, ambaye alifika
ofisini kwa Waziri huyo kwa lengo la kujitambulisha baada ya kuwasili
nchini mwishoni mwa mwaka jana.
“Karibu sana Tanzania na pia
nakupongeza sana kwa kuteuliwa katika nafasi hii, natumai kupitia
Shirika lako hapa nchini tutafanya kazi vizuri kwa kuzingatia sera,
sheria na vipaumbele vya serikali katika utendaji wako,” alisema
Masauni.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi huyo, Mahoua, pia
alimpongeza Waziri huyo kwa kuteuliwa kwenye nafasi hiyo kuiongoza
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
“Nakupongeza Mheshimiwa Waziri
kwa kuteuliwa kwa kuteuliwa kuwa Waziri na pia naipongeza Tanzania kwa
ukarimu wake wa kuendelea kupokea na kuhifadhi wakimbizi kwa miaka mingi
sasa na naomba muendelee kufanya hivyo,” alisema Mahoua.
Pia
Mwakilishi Mkazi huyo alimuhakikishia Waziri kuendeleza ushirikiano
katika shughuli za hifadhi ya wakimbizi na UNHCR itaendelea kushirikiana
na Serikali ya Tanzania katika kuwahudumia Wakimbizi.