Denmark imesema Alhamisi kwamba itaanza kuondoa vikosi vyake nchini Mali baada ya utawala wa kijeshi uliofanya mapinduzi nchini humo mapema wiki hii kuitisha kuondoka kwao likionekana kuwa pigo kwa Ufransa ambayo inaongoza operesheni ya pamoja dhidi wanamgambo wa kiislamu nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, hatua hiyo imekuja wakati utawala huo wa kijeshi ukizozana na washirika wa kimataifa pamoja na kieneo ukiwemo Umoja wa Ulaya ambao imewekea taifa hilo vikwazo kutokana na kutoitisha uchaguzi mwezi ujao kama ilivyokubaliwa.
Hali ya taharuki pia imetanda kutokana na madai kwamba serikali hiyo imeitisha mamluki wa kijeshi kutoka kampuni ya Wagner ya Russia, suala ambalo baadhi ya mataifa ya EU yamesema haliendeni mikataba ya kimataifa.
Denmark Januari 18 ilituma wanajeshi wake 105 nchini Mali ili kujiunga na kisosi maalum cha Ulaya kwa jina Takuba kilichobuniwa ili kukabiliana na wanamgambo wa kiislamu nchini humo. Denmark inasema kwamba ilileta kikosi hicho maalum kwa mwaliko wa Mali.