Wakuu wa mikoa nchini wamepewa siku 14 kupeleka taarifa za halmashauri zao ambazo zimeshindwa kufikia malengo katika makusanyo ya mapato.
Agizo hilo limetolewa leo Ijumaa Januari 28, 2022 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa wakati akitoa taarifa za mapato na matumizi kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2021.
Kwenye taarifa za makusanyo hayo Halmashauri ya Hanang' imeongoza kwa kundi la halmashauri huku Kahama ikiongoza kundi la Manispaa, Mbulu kwa kundi la miji na Tanga imeongoza kwa Majiji.
Bashungwa ametoa sababu za kuwapa maagizo hayo wakuu wa mikoa akieleza kuwa wao ndiyo wasimamizi wakuu katika maeneo yao.
Miongoni mwa maeneo wanayotakiwa kutolea taarifa ni kwa nini Wakurugenzi wa halmashauri zao wameshindwa kufikia malengo ya makusanyo na waeleze mikakati yao namna gani wanatoka walipo.
Waziri huyo ambaye leo ilikuwa mara ya kwanza kutoa taarifa ya mapato kwa halmashauri tangu alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, amesema kipimo kwa Wakurugenzi kitakuwa ni makusanyo na matumizi kwa maeneo yao.
Amemuagiza Katibu mkuu wa Wizara hiyo kukamilisha mifumo yote inayohusu malipo na makusanyo ili ifikapo Julai Mosi 2022 ianze kutumika kwa lengo la kuondoa malalamiko na mapungufu"Wakuu wa mikoa katika maeneo husika naagiza ndani ya siku 14 kuanzia leo wawe wametoa taarifa Kwa Katibu Mkuu wa Tamisemi kwa mapungufu hayo pamoja na mapendekezo ya nini kifanyike," amesema Bashungwa