Katavi. Mwanafunzi mmoja amefariki dunia na wengine 16 wamejeruhiwa baada ya kupigwa radi katika shule ya msingi ya Sokoine iliyopo kata ya Katumba Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi.
Akizungumza leo Januari 28, 2022 kwenye kikao cha baraza la madiwani Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nsimbo, Tabia Nzowa wanafunzi hao walipigwa radi juzi Jumatano.
Nzowa amesema ofisi yake ilipokea taarifa hizo kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo, Peter Belcham kuwa kati ya wanafunzi hao mwanafunzi wa darasa la tatu, Yunia Roben (10) alifariki dunia kabla ya kupata matibabu.
“Mvua hiyo ilinyesha Januari 26 jioni watoto hao wakapigwa radi wakiwa shuleni, nilipopata taarifa nilituma gari ikiwachukua kuwapeleka kituo cha afya Katumba,” amesema Nzowa.
“Kwa bahati mbaya mtoto mmoja alifariki kabla ya kupatiwa matibabu, wengine walipata matibabu na walirejea nyumbani,” amesema Nzowa
Akizungumza na Mwananchi leo mwalimu mkuu wa shule hiyo, Peter Belcham amesema mvua hiyo haikuwa kubwa lakini ilikuwa ya mawe ikiambatana na upepo