Bodi ya utalii Tanzania (TTB) imeapokea
maandamano ya Wanachama wa Umoja wa Vijana –UVCCM Tanzania Kata ya
Saranga iliyopo katika Jimbo la Kibamba, Wilaya ya Ubungo Jijini Dar es
Salaam ya kuhamasisha Utalii wa ndani hasa wa kupanda Mlima Kilimanjaro.
Maandamano hayo yaliyoanzia katika kata ya Saranga na kupokelewa katika
Export Processing Zones Authority (EPZA) na Kaimu Mkurugenzi mkuu wa
TTB Bw. Felix John.
Vijana hao ambao wamesema wanatekeleza ilani
ya chama hicho ya kuvutia Watalii wa ndani na kuongeza pato la Taifa
kupitia sekta hiyo, wameamua kuutangaza Mlima Kilimanjaro kama sehemu ya
maadhimisho ya miaka 45 tangu kuanzishwa kwa CCM.
Akizungumza
mara baada ya kupokea maandamano hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TTB Bw.
Felix John amesema, mchango wa sekta ya utalii katika kukuza ajira kwa
vijana ni mkubwa hivyo kufanyika kwa maandamano haya ya kuutangaza
utalii ni sehemu mojawapo ya kuchochea uchumi wa Taifa , hivyo
tunawapongeza vijana hawa kutuunga mkono katika kutangaza vivutio
vyetu”.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Saranga Bw.
Ally Adam Chinangu amesema “wameamua kuitangazia Dunia kuwa Mlima
Kilimanjaro ni mali ya Tanzania, pamoja na kuwa unaweza kuuona ukiwa
kwenye nchi jirani, Sisi vijana tunasema tuijulishe dunia kama Mlima
Kilimanjaro upo nchini Tanzania”.
Nao baadhi ya washiriki
wanawake katika maandamano hayo kutoka Bodi ya Utalii Tanzania na UVCCM
Kata ya Saranga, wametumia fursa ya maandamano hayo kuhamasisha Wanawake
kutumia siku ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani inayoadhimishwa
tarehe 8 mwezi wa tatu ya kila mwaka kutembelea vivutio vya Utalii
vilivyopo nchini.
TTB inaendelea na juhudi za kuhamasisha utalii
kwa makundi mbalimbali ya kijamii yakiwepo ya Vijana, Wawake, Wanafunzi
na mengine mengi, katika kutembelea vivutio vya utalii na kuvitangaza
ili kuvutia Watanzania kujenga utamaduni wa kuvitembelea vivutio hivyo.