Rais Yoweri Museveni wa Uganda amepinga uamuzi wa Askofu wa kanisa la Uganda la kuwazuia wasichana wajawazito kurudi shuleni baada ya shule kufunguliwa mwezi huu nchini Uganda
Hii ni kutokana na janga la Covid- 19 ambapo shule zilifungwa nchini kwa kipindi cha miaka 2 huku wasichana wengi wakipata ujauzito.
Askofu wa Kanisa la Uganda Dayosisi ya Mukono James Ssebgala aliwaamuru walimu wa shule zinazomilikiwa na Kanisa la Uganda zisiwaruhusu wanafunzi wajawazito kurudi shule baada ya shule kufunguliwa nchini Uganda tarehe 10 mwezi wa Januari mwaka huu.
Askofu huyo alipinga mpango wa wizara ya elimu nchini Uganda wa kuwaruhusu wanafunzi wote waliobeba mimba na wale waliojifungua wakati wa zuio la kukaa nyumbani karibu miaka miwili warudi shuleni kuendelea na masomo.
Aliwataka walimu kuwapeleka wanafunzi katika vituo vya afya wapimwe kabla ya kuanza na masomo yule akayepatikana na mimba wamurudishe nyumbani.
Katika hotuba yake Rais Museveni kwa taifa hapo jana siku ya kuanzimisha miaka 36 ya chama chake cha NRM kuingia madarakani ,amepinga agizo la .
”Kitu ambacho naweza kukwambia wazi nisichokubaliana nacho , ni kumlaumu msichana asiendelee na masomo kwa sababu alipata ujauzito kwa mara ya kwanza, siwezi kukubalina na hilo hata katika masuala ya kidini, kwa sababu mtoto kama alifanya makosa huwezi kumlaani katika maisha yake yote na kumkatisha masomo yake.
”Mbona kuna mama wazee zaidi ya miaka 50 wanarudi shuleni kusoma? kwanini umkatize mtoto masomo wakati alipata matatizo”.Alihoji Rais Museveni.
Tangu shule zifunguliwe nchini Uganda tarhe 10 mwezi huu kulingana na takwimu za wizara ya elimu kati ya wanafunzi milioni 15 kote nchini kabla ya zuio la janga la corona aslilimia 30% ya wanafunzi hao hawajarudi shuleni wengine kutokana na ujauzito na kujifungua na wengine wazazi kushindwa kulipa karo za shule.