Watu wawili wamekufa na wengine kadhaa wamejeruhiwa jana jioni mjini Monrovia baada ya gari kuwagonga wafuasi wa Joseph Boakai, saa chache kabla ya kutangazwa kwake kuwa mshindi wa urais nchini Liberia.
Dereva wa gari hiyo alitoroka maramoja baada ya tukio hilo. Polisi hawajatangaza sababu ziliziopelekea mkasa huo lakini msemaji wa Boakai amesema hana shaka kuwa ni kitendo cha makusudi.Mwanasiasa mkongwe nchini Liberia Joseph Boakai alimshinda rais aliyekuwa madarakani na nyota wa zamani wa soka George Weah kwa asilimia 50.64 ya kura dhidi ya asilimia 49.36 katika uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba 14 mwaka huu. Serikali ya Weah imekuwa ikishutumiwa kwa vitendo vya rushwa na kushindwa kutimiza ahadi yake ya kuboresha maisha ya watu maskini zaidi.