Mkuu wa Majeshi ya Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba ametangaza kutolewa kwa amri mpya kwa wanajeshi wa nchi hiyo kumkamata mwanasiasa wa upinzani, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine akiwa hai au amekufa.
Kupitia ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, Jenerali Muhoozi amesema operesheni za kumtafuta Bobi Wine zilisitishwa kwa muda wa saa 24 kwa maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi Rais Yoweri Museveni aliyeshinda uchaguzi wa hivi karibuni na kuchaguliwa kwa muhula wa saba kuiongoza Uganda.
Muhoozi amesema kusitishwa huko kulilenga kumpa Bobi Wine fursa ya kujisalimisha kwa amani lakini baada ya kushindwa kufanya hivyo ndani ya muda uliotolewa, operesheni za kijeshi zimeendelea rasmi.
Bobi Wine amekuwa mafichoni tangu kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi akidai kuwepo kwa njama ya kutaka kumdhuru.
Wiki iliyopita Muhoozi alimpa muda wa saa 48 kujisalimisha kwa Polisi hata hivyo hakufanya hivyo na jitihada za kumtafuta zimeendelea bila mafanikio.
Inaelezwa kuwa Bobi Wine aliondoka nyumbani kwake siku ya Ijumaa tarehe 16 ya mwezi huu baada ya wanajeshi kufika eneo hilo siku moja kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.
Katika uchaguzi huo Rais Museveni alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 71 ya kura huku Bobi Wine akipata asilimia 24.
Akizungumzia suala hilo,Muhoozi amesema:
“Tulisitisha utafutaji wa Kabobi kwa saa 24 kwa maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu.
Ilionekana angetaka kujisalimisha kwa amani, lakini hajafanya hivyo.
Sasa askari wetu wamepewa amri ya kumkamata akiwa hai au akiwa amekufa.”
Aidha amekanusha madai ya askari kumshambulia mke wa Bobi Wine, Barbie Kyagulanyi, akisisitiza kuwa jeshi halina utaratibu wa kuwaumiza wanawake, na kwamba lengo ni kumtafuta Bobi Wine mwenyewe.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime