Maseneta Wachunguza Ufisadi Kaunti za Pwani

Magavana wanne wa eneo la Pwani wamejikuta katika shinikizo kali baada ya Seneti kuanzisha uchunguzi kuhusu madai ya uozo wa kifedha, ufisadi na ukiukaji wa sheria hasa katika sekta nyeti za maji na afya.

Magavana hao—Abdulswamad Nassir (Mombasa), Gideon Mung’aro (Kilifi), Issa Timamy (Lamu) na Dhado Godhana (Tana River)—walifika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uwekezaji wa Kaunti ambako walishindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu matumizi ya mabilioni ya fedha za umma.

Katika vikao vilivyofanyika Nairobi wiki iliyopita maseneta walihoji kwa nini fedha nyingi zilitumika bila stakabadhi au zikatumika vibaya katika hospitali za kaunti na mashirika ya kusambaza maji ambapo kamati ilieleza wasiwasi kuwa mifumo ya kifedha katika kaunti hizo imekuwa ikikiukwa kwa miaka bila hatua za kurekebisha.

Hata hivyo Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Nassir, alikabiliwa na maswali makali baada ya kubainika kuwa Hospitali Kuu ya Mafunzo na Rufaa ya Pwani (CGTRH) imekuwa ikikaidi sheria kwa kushindwa kuwasilisha ripoti za kifedha kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

“Hii imekuwa desturi. Kila mwaka hospitali hii inapuuzia afisi ya mkaguzi wa fedha za umma,” alisema mwenyekiti wa kamati, Seneta Godfrey Osotsi.

Seneta Eddy Oketch (Migori) alitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya uongozi wa hospitali hiyo. Gavana Nassir alisema maafisa wawili tayari wamesimamishwa kazi.

Uchunguzi pia ulifichua hali mbaya katika Kampuni ya Maji ya Mombasa (MOWASCO), ambayo imefilisika ikiwa na deni la Sh2.26 bilioni.

Maseneta walishangazwa kubaini kuwa majitaka yanaachiliwa moja kwa moja baharini kutokana na mitambo ya kusafisha maji taka kutofanya kazi.

Seneta Peris Tobiko alitaja hali hiyo kuwa uchafuzi wa mazingira na ukiukaji wa haki za binadamu, akionya kuwa maisha ya umma yako hatarini.

Gavana Nassir alijitetea akisema miradi ya ukarabati inayofadhiliwa na Benki ya Dunia inaendelea na inatarajiwa kukamilika Oktoba 2026, maelezo ambayo kamati ilikataa, ikitaka hatua za dharura zichukuliwe.

Kwa upande wa Kilifi, Gavana Gideon Mung’aro alihojiwa kuhusu ongezeko kubwa la maji yanayotumiwa bila kulipiwa katika Malindi Water.

Ripoti ya mkaguzi wa hesabu inaonyesha kuwa maji yasiyolipiwa yaliongezeka kutoka asilimia 16 hadi 42 ndani ya mwaka mmoja.

“Hili si jambo la kawaida. Huu ni wizi wa makusudi,” alisema Seneta Osotsi.

Kamati ilikataa ombi la gavana la kupewa muda zaidi, ikisema mashirika ya maji yamegeuka kuwa mashimo ya kupotezea fedha za umma.

Gavana wa Lamu, Issa Timamy, alitakiwa kuelezea kwa nini hoja za ukaguzi zimekuwa zikijirudia katika hospitali za Faza, Mpeketoni na Hospitali ya Rufaa ya Lamu.

Kamati ilibaini ukosefu wa stakabadhi za matumizi ya fedha na usimamizi dhaifu wa mali za kaunti.

Seneta Agnes Kavindu (Machakos) alieleza wasiwasi kuwa miradi mingi ya maendeleo katika kaunti hiyo imekwama tangu 2023 huku rekodi za kifedha zikiwa na makosa ya msingi.

Gavana wa Tana River, Dhado Godhana, aliahidi kushirikiana na taasisi za ukaguzi ili kuboresha uwajibikaji wa kifedha.

Kwa upande wa Kwale, Gavana Fatuma Achani alihojiwa kuhusu usimamizi wa manispaa, huku akilalamikia uhaba wa wafanyakazi katika hospitali za kaunti na shule za chekechea.

Kamati ya Seneti ilionya kuwa haitasita kupendekeza hatua za kisheria dhidi ya maafisa wa kaunti watakaobainika kuhusika na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Uchunguzi huo unaendelea huku maseneta wakisisitiza kuwa uwajibikaji katika sekta za maji na afya hauwezi kuahirishwa kwa sababu unagusa moja kwa moja maisha ya wananchi.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii