Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wako nchini India kwa ziara itakayoshuhudia kutiwa saini mkataba wa biashara huria baina ya pande hizo mbili ambao mashauriano yake yamefanyika kwa karibu miaka 20.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen na mwenzake wa Baraza Kuu la umoja huo Antonio Costa waliwasili kwenye mji mkuu wa India, New Delhi, jana Jumapili kutia saini mkataba huo ambao Umoja wa Ulaya umeutaja kuwa "mama wa mikataba yote ya biashara huria" duniani.
Hii leo viongozi hao wawili watakuwa wageni wa heshima kwenye sherehe za siku ya Jamhuri kabla ya hapo kesho kushiriki mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na India utakaojumuisha kutiwa saini mkataba huo wa biashara.
Umoja wa Ulaya unaizingatia India kuwa eneo muhimu kibiashara hasa ikizingatiwa kuwa taifa hilo la Asia lina idadi kubwa zaidi ya watu duniani na uchumi wake unakua kwa kasi.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime