Wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa wameonya kuwa kuongezeka kwa vurugu nchini Sudan Kusini kunaongeza hatari ya ukatili mkubwa dhidi ya raia kufuatia mapigano mapya na matamko ya uchochezi kutoka kwa viongozi wa kijeshi.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumapili Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ilieleza kuwa ina wasiwasi mkubwa na mapigano yanayoendelea katika Jimbo la Jonglei, kaskazini mwa mji mkuu Juba ambapo Mashahidi wameripoti raia wakikimbia makazi yao na kukimbilia kwenye vinamasi vilivyo karibu ili kujiokoa.
Ambapo hali hiyo imechochewa zaidi na matamshi ya msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini (SSPDF) Lul Ruai Koang aliyewataka wakazi wa Jonglei kuondoka mara moja katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa SPLA-IO. Alionya kuwa raia waliobaki katika maeneo hayo watachukuliwa kama malengo halali ya kijeshi.
Hivyo tume ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa matamko ya makamanda yanayohamasisha vurugu dhidi ya raia, sambamba na uhamasishaji wa wanajeshi, yanaongeza hatari katika kipindi ambacho mchakato wa amani tayari umedhoofika.
Mkuu wa Jeshi, Paul Nang Majok, aliripotiwa kuamuru wanajeshi “kuangamiza uasi” ndani ya siku saba kauli ambayo imezua hofu zaidi miongoni mwa wananchi.
Aidha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo (UNMISS) nao umeeleza wasiwasi wake mkubwa, ukisisitiza kuwa matamshi ya uchochezi yanayolenga raia, hususan makundi yaliyo hatarini hayakubaliki na yanapaswa kusitishwa mara moja.
Hata hivyo kwa mujibu wa mamlaka za Sudan Kusini, mapigano mapya yamesababisha zaidi ya watu 180,000 kuyakimbia makazi yao. Nchi hiyo imeendelea kukumbwa na migogoro, umaskini na ufisadi tangu kupata uhuru mwaka 2011, huku juhudi za amani zikidorora baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya kugawana madaraka kati ya Rais Salva Kiir na mpinzani wake Riek Machar.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime