Bodi ya Nyama Yafunga Machinjio ya Muheza kwa Kuhatarisha Afya

Bodi ya Nyama Kanda ya Kaskazini imeyafunga machinjio ya Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, kwa muda usiojulikana kufuatia ukiukaji wa kanuni za afya na usalama wa walaji.

Machinjio hayo yaliyopo Kijiji cha Sega yalifungwa baada ya ukaguzi wa kushtukiza kubaini kuwa miundombinu yake, hususan sakafu, imechakaa vibaya na uchinjaji unaendelea bila kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Muheza, Salimu Sechambo, amethibitisha kufungwa kwa machinjio hayo, akisema hatua hiyo ilichukuliwa na Bodi ya Nyama Kanda ya Kaskazini mara baada ya kubaini kasoro kubwa.

Amesema halmashauri imeanza kuchukua hatua za haraka kurekebisha miundombinu hiyo ili huduma za uchinjaji zirudi kama kawaida.

Sechambo amewatoa hofu wafanyabiashara wa nyama na walaji, akisisitiza kuwa matengenezo yanafanyika kwa kasi na huduma itarejea mara tu masharti yatakapotekelezwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wachinjaji Wilaya ya Muheza, Oimar Lutika, ameomba halmashauri iharakishe ukarabati wa machinjio hayo akisema kufungwa kwake kumeathiri shughuli za biashara na upatikanaji wa nyama kwa wananchi.

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Muheza, Hamis Mwinjuma (MwanaFA), alifanya ziara katika machinjio hayo na kubaini hali duni ya miundombinu.

Katika ziara hiyo, Mwinjuma alieleza kusikitishwa na hali ya machinjio, akibainisha kuwa miundombinu iliyopo ni hatarishi kwa afya ya jamii, huku jitihada zilizokuwa zimefanyika za ukarabati akizitaja kuwa hazikidhi viwango wala ubora unaohitajika.

Bodi ya Nyama imesisitiza kuwa machinjio hayo yataendelea kufungwa hadi pale halmashauri itakapotekeleza kikamilifu masharti ya afya na usalama, ikiwemo kuboresha miundombinu na kufuata kanuni za uchinjaji.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii