Ajira Haramu: Jinsi Kaunti 41 Zilivyopuuza Sheria na Kujaza Mfumo kwa Wafanyakazi

Uchunguzi wa kina wa ripoti za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali umebaini mtandao mpana wa ukiukaji wa sheria za ajira katika serikali za kaunti ambapo wafanyakazi 27,284 waliajiriwa kinyume cha sheria katika kaunti 41 ndani ya kipindi cha miaka mitatu hadi Juni 2024.

Ripoti hizo zinaonyesha picha ya mfumo uliopuuzwa makusudi ambapo magavana na maafisa wakuu wa kaunti waliendesha ajira bila mipango bila bajeti na mara nyingine bila kufuata taratibu za msingi za uwazi na ushindani.

Kati ya mwaka wa kifedha 2021/22 hadi 2023/24, kaunti nyingi ziliendelea kuajiri wafanyakazi licha ya kukosa mipango ya kila mwaka ya ajira—hitaji la kisheria linalopaswa kuongoza idadi, aina na gharama za wafanyakazi.

Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, anaonya kuwa kukosekana kwa mipango hiyo kunafungua mianya ya kuajiri wafanyakazi kupita kiasi, kuajiri kwa upendeleo, au kujaza nyadhifa zisizoendana na mahitaji halisi ya wananchi.

Uchunguzi unaonyesha kuwa Uasin Gishu ndiyo iliyoongoza kwa ajira haramu, ikiajiri wafanyakazi 3,982 bila kuwepo kwa mipango ya ajira ya kuhalalisha zoezi hilo.

Asilimia 14.6 ya ajira zote haramu katika kaunti 41 zilifanyika katika kaunti hiyo moja pekee. Mzigo wa mishahara ulifikia wastani wa asilimia 41.7, ukiukaji wa wazi wa kiwango cha kisheria cha asilimia 35.

“Idara zilizofanya uajiri hazikuwa na mipango ya kila mwaka ya ajira,” anasema Mkaguzi wa Hesabu, akionya kuwa hali hiyo inaweza kuathiri uthabiti wa kifedha wa kaunti.

Ripoti za ukaguzi zinafichua mifumo inayojirudia ya ukiukaji wa taratibu, ikiwemo:

  • Kuajiri bila kutangaza nafasi

  • Kuwateua watu ambao hawakuomba ajira

  • Kuhalalisha bajeti baada ya ajira kufanyika

  • Uteuzi wa moja kwa moja bila ushindani

Katika Narok, Mkaguzi wa Hesabu alibaini kuwa mchakato mzima wa ajira ulikuwa na “udhaifu mwingi,” hali inayozorotesha uwazi na haki.

Katika Embu, gavana alianzisha ofisi za kasisi wa kaunti na mshauri wa afya wa gavana bila msingi wa kisheria. Nafasi hizo zilijazwa bila kuzingatia mapendekezo ya Kamati ya Ushauri ya Usimamizi wa Wafanyakazi ya Kaunti.

Kaunti ya Lamu iliajiri wafanyakazi 100 bila tathmini ya mahitaji, huku 16 wakiajiriwa kabla hata ya matangazo kutolewa.

Katika Samburu, wafanyakazi 746 waliajiriwa, ambapo 192 waliteuliwa moja kwa moja na kulipwa Sh47.7 milioni ndani ya miaka mitatu—bila ushindani wala uthibitisho wa mahitaji.

Uchunguzi unaonyesha kuwa kaunti 10 pekee zilichangia zaidi ya nusu ya ajira zote mpya, zikiajiri wafanyakazi 13,696. Mbali na Uasin Gishu, kaunti kama Kitui, Trans Nzoia, Turkana, Bomet, Nyamira, Nakuru, Nairobi, Narok na Laikipia zilitajwa.

Licha ya ukubwa wa ukiukaji huo, ripoti zinaonyesha udhaifu wa utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi. Hakuna ushahidi wa wazi wa kuwajibishwa kwa maafisa waliohusika, huku ajira nyingi zikiendelea kubebesha walipa kodi mzigo wa mishahara.

Aidha wataalamu wa utawala wa umma wanaonya kuwa endapo hatua hazitachukuliwa, kaunti zitazidi kuwa na wafanyakazi wengi katika idara zisizo na tija huku huduma muhimu zikidorora.

Hata hivyo kwa mujibu wa Mkaguzi wa Hesabu, kuajiri bila mipango, bila bajeti na bila uwazi si tu uzembe—ni hatari kwa uhai wa ugatuzi. Bila uwajibikaji, mfumo wa ajira katika kaunti unaendelea kutekwa kwa maslahi ya kisiasa kwa gharama ya wananchi.


#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii