Rwanda kufungua mpaka wa Gatuna kati yake na Uganda

Mpaka baina ya Rwanda na Uganda ulifungwa mwaka 2019 kufuatia mzozo huo, na kukwamisha shuguli za kijamii na kibiashara baina ya mataifa hayo jirani.
Taarifa hiyo imetolewa siku kadhaa baada ya ziara ya mtoto wa rais wa Uganda Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba nchini Rwanda tarehe 22 mwezi Januari.
Taarifa hiyo imesema kuwa serikali ya Rwanda imetambua kuwa kuna mchakato wa kutatua masuala yaliyoibuliwa na Rwanda pamoja na ahadi zilizotolewa na serikali ya Uganda kukabiliana na vikwazo vilivyosalia.
''Kutokana na hayo na yale yaliyokuwepo kwenye taarifa ya pamoja ya mkutano wa nne wa mataifa manne uliofanyika Gatuna tarehe 21 mwezi Februari mwaka 2020, Serikali ya Rwanda inapenda kuujulisha Umma kuwa mpaka wa Gatuna wa kati ya Rwanda na Uganda utafunguliwa tena tarehe 31 mwezi Januari mwaka 2022.'' Ilisema taarifa hiyo.
Kwa hali ilivyo kwa vituo vingine vya mpaka wa ardhi nchini, mamlaka ya afya ya Rwanda na Uganda zitafanya kazi pamoja kuweka hatua muhimu za kuchukua wakati huu wa mapambano dhidi ya Covid-19.
Serikali ya Rwanda imesema bado imejizatiti katika juhudi zinazoendelea za kutatua masuala mbalimbali kati ya Rwanda na Uganda na inaamini kuwa tangazo la leo litachangia kwa kiasi kikubwa katika kuharakisha kurejesha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Naibu msemaji mkuu wa serikali ya Rwanda anasema mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa juma baina ya Luteni Jenerali wa Uganda Muhoozi Kainerugaba na Rais Paul Kagame mjini Kigali yanatoa matumaini ya 50% ya suluhu ya mzozo baina ya nchi hizo.
Akizungumza na BBC, Bw Alain Mukuralinda, alisema viongozi hao walielezana ukweli na kuwa wazi juu ya masuala yanayosababisha kuzorota kwa uhusiano wa nchi mbili.
'' Walisema tumezungumzia juu ya wasi wasi uliooneshwa na Rwanda, hofu nazoweza kusema ni mbili…moja ni tatizo la Wanyarwanda wanaonyanyaswa wakiwa Uganda na kupigwa, kunyang'anywa mali zao, na kisha kufukuzwa na kuletwa mpakani…Kuna wapinzani wa utawala wa Rwanda waliopo katika eneo la Uganda na walioko maeneo mengine wanaosaidiwa kutoka Uganda''.
Hii ina maanisha kuwa kuna hatua zitakazochukuliwa ili haya yote yaishe.Rais wa Angola João Lourenço (wa pili kulia) na Etienne Tshisekedi wa Congo (wa kwanza kulia) walisimamia mazungumzo kati ya Uganda na Rwanda.
Akijibu swali juu ya iwapo shutuma za Uganda dhidi ya Rwanda kuwa inaunga mkono harakati za kuvuruga usalama wake na kuingilia ngazi zake za usalama, Bw Alain Mukuralinda amesema ''Sidhani waliketi kujadili tofauti zao, na kama Uganda ilionyesha ushahidi wa shutuma zake basi sina shaka hilo lilijadiliwa…kama kuna mambo ambayo Uganda inailaumu Rwanda sidhani kama hayakujadiliwa .''
Msemaji huyo wa Rwanda amesema anaweza kusema 50% ya suluhu ya tatizo la uhusiano baina ya Rwanda imepatikana kwa sasa, na 50% iliyobakia ni ya utekelezwaji wa yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo.
Bw Mukuralinda, alisema kuwa kuna matumaini makubwa ya kutatuliwa kwa mzozo baina ya nchi mbili, ikizingatiwa kuwa mjumbe alifanya mazungumzo na Rais Kagame ni wa ngazi ya juu zaidi, mtoto wa kwanza wa Rais na mshauri wake, na Mkuu wa majeshi ya ardhini.
Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba ni mtoto wa kiume wa rais Yoweri Museveni, mshauri wake mkuu na Kamanda mkuu wa vikosi vya ardhini , na ziara yake nchini Rwanda inaangaliwa kama hatua kubwa kubwa katika kurejesha uhusiano mwema baina ya nchi hizo mbili.
Kila upande ulikuwa ukiulaumu upande mwingine kuwa chanzo cha kuzorota kwa mahusiano ya pande mbili.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii