Waziri wa Mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema leo kuwa
Moscow haitaki vita na Ukraine, huku akionyesha matumaini kuhusu
mapendekezo ya usalama yaliyowasilishwa na Marekani. Lavrov amesema
mapendekezo ya Marekani yalikuwa bora zaidi kuliko yaliyowasilishwa na
Juamuiya ya Kujihami ya NATO. Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Urusi
amesema anatarajia kukutana na mwenzake wa Marekani Antony Blinken
katika wiki chache zijazo. Lavrov amesema Rais Vladmir Putin ataamua
jinsi ya kuyajibu mapendekezo hayo. Hapo jana, Rais Joe Biden
amesisitiza kwamba Marekani pamoja na washirika wake wataendelea kuiunga
mkono Ukraine ili kuweza kujibu kwa ufanisi ikiwa Urusi itaivamia nchi
hiyo. Rais Biden amesema hayo katika mazungumzo yake na rais wa Ukraine
Volodymyr Zelenksy waliyoyafanya kwa njia ya simu.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii