Takriban wahamiaji sita wamekufa maji na wengine 30 hawajulikani walipo baada ya mashua waliyokuwa wamepanda kupinduka katika pwani ya Tunisia.
Watu 34 waliokolewa na wanamaji wa Tunisia na meli za walinzi wa pwani.
Walionusurika walisema wahamiaji 70 walikuwa wamepanda mashua hiyo kutoka mataifa mbalimbali zikiwemo Misri, Sudan na Morocco.
Msemaji wa jeshi la ulinzi wa Tunisia alisema wameondoka Libya na walikuwa na matumaini ya kufika Ulaya.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linasema kuwa katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka jana, wahamiaji wasiopungua 1,300 walitoweka au kufa maji wakijaribu kuvuka kutoka Afrika Kaskazini kuelekea Italia.