Ubalozi wa Ufaransa nchini Kenya umeonya kuhusu tishio la shambulizi la kigaidi dhidi ya raia wa Magharibi wanaoishi nchini Kenya.
Katika tahadhari siku ya Alhamisi, ubalozi wa Ufaransa uliwaonya raia wake kuwa waangalifu zaidi.
Ilisema kuna "kuendelea kwa vitisho vikali" na hatari ya maeneo ya umma, yanayotembelewa na raia wa kigeni kulengwa.
Ilitaja migahawa na hoteli, kumbi za starehe, maduka makubwa hasa katika mji mkuu Nairobi - na kushauri watu kuepuka kuzitembelea ikiwa ni pamoja na mwishoni mwa juma hili. Balozi za Uholanzi na Ujerumani pia zimewataka raia wao kuwa macho.