Zaidi ya watu 1,000 wamekusanyika katika uwanja mkuu katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou, kusherehekea mapinduzi ya Jumatatu, huku wengine wakichoma bendera ya Ufaransa na wengine wakicheza muziki unaopigwa, shirika la habari la Reuters linaripoti.
Kuchomwa kwa bendera ya Ufaransa ni ishara ya hivi punde zaidi ya kuongezeka kwa mfadhaiko kuhusu jukumu la kijeshi la mkoloni huyo wa zamani katika eneo hilo.
Ufaransa ina wanajeshi nchini Burkina Faso na katika mataifa mengine kadhaa ya Afrika Magharibi ili kusaidia kupambana na wanamgambo wa kijihadi ambao wamekuwa wakisababisha uharibifu katika eneo hilo.
Lakini uwepo wa wanajeshi wake umeonekana kuwa na utata, kama mchambuzi Paul Melly alivyoeleza katika makala ya hivi majuzi ya BBC.
Jeshi nchini Burkina Faso lilisema limetwaa mamlaka kwa sababu ya kushindwa kwa Rais Roch Kaboré kuliunganisha taifa na kukabiliana vilivyo na mzozo wa usalama ambao "unatishia misingi ya taifa letu".
Jeshi katika nchi jirani ya Mali lilitoa sababu sawa na hilo lilipochukuwa mamlaka mnamo Mei 2021 - mapinduzi ambayo yalipokelewa kwa furaha na umma licha ya kulaaniwa kimataifa.
Huko Ouagadougou, baadhi ya watu pia walikosoa Jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi Ecowas, ambayo inashikilia msimamo mkali dhidi ya mapinduzi.
"Ecowas haitujali, na jumuiya ya kimataifa inataka tu kulaani," muandamanaji Armel Ouedraogo.