Wafuasi wa jeshi nchini Burkina Faso wameandamana katika mji mkuu jana Jumanne, siku moja baada ya maafisa jeshi kumkamata rais Roch Kabore na kuivunja serikali ya nchi hiyo.
Mamia kadhaa ya watu walikusanyika katikati mwa mji mkuu Ouagadougou, huku wakipeperusha bendera na kupiga honi katika kuunga utawala mpya wa kijeshi.
Serikali ya Kabore imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kuhusiana na namna inavyoshughulikia wapiganaji wa Kiislamu, wanaofanya mashambulizi ya mara kwa mara na kusababisha vifo vya mamia ya watu.
Kabore alichaguliwa kwa mara ya kwanza 2015, na kushinda muhula wa pili mwaka 2020. Amekuwa akikabiliwa na maandamano ya mara kwa mara kumtaka ajiuzulu. Hatua ya jeshi kutwaa madara siku ya Jumatatu ilitanguliwa na siku kadhaa za maandamano dhidi ya serikali ya Kabore.