KESI YA SABAYA NA WENZAKE KILINDIMA TENA LEO.

Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita inatarajiwa kuendelea leo kwa shahidi wa 14 wa upande wa mashataka kuanza kutoa ushahidi.

Sabaya na wenzake wanatuhumiwa kwa utakatishaji fedha na kujipatia rushwa ya Sh90 milioni. Kesi inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha mbele ya Hakimu Mkazim Patricia Kisinda.

Januari 7, Hakimu Kisinda aliahirisha kesi hiyo baada ya shahidi wa 13, Ofisa Uchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), Ramadhan Juma kumaliza kuhojiwa na mawakili wa utetezi.

Katika kesi hiyo namba 27 ya mwaka 2021, mbali na Sabaya watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Wanadaiwa mashtaka matano likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na kutakatisha fedha Sh 90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso, huku wakijua kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.

Kosa la pili, tatu na nne Sabaya pekee anadaiwa kujihusisha na rushwa ambapo alichukua Sh90 milioni na matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii