Huku wakivalia vazi lao la kitamaduni la jamii ya Maasai na kuzungukwa na ng'ombe, nyota wapya wa Tanzania katika mtandao wa TikTok ambao ni ndugu Kili na Neema Paul, wanajiandaa kurekodi video yao hivi karibuni.
Simu ya smartphone inawekwa kwenye tripod mita chache mbali kutoka kwenye nyumba yao iliyopo katika Kijiji kidogo cha Mindu Tulieni, mashariki mwa jimbo la Pwani.
Mji uliopo jirani ni Lugoba, uko umbali wa saa moja kwa mwendo wa miguu. Kutokana na ukosefu wa umeme kijijini, Kili hulazimika kutembelea mjini ili kuchaji simu yake.
Wanajipanga vyema mbele ya kamera, Kili mwenye umri wa miaka 26, anasimama nyuma kidogo ya dada yake Neema, mwenye umri wa miaka 23 .
Mara muziki unapoanza, ndugu hawa hugeuza midomo yao kuwa sawa kabisa na ile inayoonekana katika baadhi ya nyimbo na densi maarufu Bollywood.
Kwa kipindi cha miezi michache iliyopita, video za uimbaji wao wa nyimbo za Kihindi kwa namna iliyo sawa kabisa na waimbaji halisi zimekuwa zikisambaa sana kote nchini India na kuibua gumzo kwenye mitandao ya kijamii.
Video yao maarufu, iliyochezwa na Rataan Lambiyan kutoka filamu ya mwaka huu ya Bollywood Shershaah, ilitazamwa na watu zaidi ya milioni moja katika kipindi cha siku chache.