Wasanii Bongofleva waliofika mjini mwaka 2021

WANASEMA kuimba kupokezana! Kila mwaka wasanii wapya huingia kwenye gemu ya muziki wa Bongofleva kama ambavyo wasanii wengine hufulia na kupotea. Na kwa sababu mwaka 2021 unaelekea ukingoni, ni vyema tutakumbushana orodha ya wasanii waliongia mjini mwaka huu.

Kuingia mjini inaweza kuwa aidha ni wasanii wapya kabisa ambao tumeanza kuwasikia kwa mara ya kwanza mwaka huu au wasanii ambao waliwahi kuwepo kwenye gemu lakini umaarufu mkubwa wameupata mwaka huu.


MAC VOICE

Mwezi Machi mwaka huu msanii Rayvanny alizindua lebo yake inayoitwa Next Level Music, na ilipofika Septemba akamtangaza msanii ‘first born’ wa lebo hiyo anayeitwa Mac Voice.


Akiwa na miezi mitatu tu kwenye gemu Mac Voice ameachia EP yenye ngoma kali nne na kujizolea umaarufu kwa namna yake.

Kingine kilichowagusa watu kuhusu yeye ni vile mashabiki wa Bongofleva wanavyomfaninisha sana na Rayvanny kuanzia sauti yake, aina ya uimbaji, mtindo wa uandishi wa mashairi na hata muonekano wake.

Licha ya upya wake kwenye gemu, Mac Voice anabebwa na namba kwani tayari ndani ya miezi hii mitatu tu amekusanya watazamaji 5 milioni kwenye chaneli yake ya YouTube na kumfanya kuwa msanii mpya mwenye ‘views’ nyingi zaidi mwaka huu.


ANJELLA

Kwa mara ya kwanza alisikika kitaifa mwezi Januari baada ya kushirikishwa kwenye wimbo wa msanii na bosi wa Konde Gang, Harmonize. Baada ya Anjella A.K.A Black Angel kuonyesha kipaji kikubwa kwenye wimbo huo, mabosi wa lebo hiyo ya pili kwa ukubwa Tanzania waliamua kumsajili na kumfanya kuwa ‘first lady’ wao, yaani msanii wa kike pekee ndani ya lebo.


Kisha miezi nane iliyopita, yaani Oktoba aliachia ngoma yake binafsi ikifuatiwa na kutambulishwa rasmi kuwa msanii wa lebo hiyo katika bonge moja la party ya kumkaribisha lililofanyika makao makuu ya Konde Gang, Mbezi Beach, Dar es Salaam.

Hadi sasa Anjella ameshaachia ngoma takribani tano zilizopata kutazamwa zaidi ya mara 13 milioni kwenye mtandao wa YouTube. Huku akaunti yake ya Instagram ikisoma kuwa nusu milioni, yote ni kuonyesha jinsi gani amejua kuingia mjini.


LODY MUSIC

Anatajwa kama msanii pekee mpya aliyeingia kwenye gemu mwaka huu bila mgongo wa lebo kubwa kama vile Wasafi, Konde Gang na Kings Music ya Alikiba wala kiki za kushindanishwa na wasanii ambao tayari wapo kwenye gemu kama ilivyokuwa kwa Anjella na Zuchu.


Lody Music alianza kupenya taratibu kwenye gemu alipoachia ngoma yake ya kuitwa Linapotea, hiyo ikiwa ni mwezi Mei mwaka huu. Lakini umaarufu zaidi aliupata alipoachia goma lake la kuitwa Kubali miezi miwili iliyopita.

Lody anatamba zaidi kwa aina yake ya muziki wa tofauti, muziki wa taratibu ambao wasanii wengi wa kisasa wanaukwepa, huku mashairi yake yakiwa yamelalia zaidi kwenye suala zima la mapenzi hususan akiimba kuhusu kutendwa na maumivu ya mapenzi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii