Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha imepanga kuanzia Februari 14, 2022 kuanza kusikiliza rufaa iliyofunguliwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili kupinga hukumu ya miaka thelathini jela.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Ruth Massam ameeleza hayo Desemba 13, 2021 wakati rufaa hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuanza kusikiliza.
Msajili amesema rufaa hiyo itasikilizwa mfulululizo kuanzia Februari 14, mwakani kupitia Jaji atakayekuwa amepewa jukumu hilo.
Lengai Ole Sabaya, Sylvester Nyegu na Daniel Mbura kupitia mawakili wao wanapinga hukumu ya Octoba 15, 2021 ya kifungo cha miaka 30 jela iliyotolewa na mahakama ya hakimu mkazi Arusha baada ya kuwatia hatiani kwa makosa matatu ikiwamo la unyang'anyi wa kutumia silaha.