Mtunzi na mwimbaji nyota wa miondoko ya Soukous, Koffi Olomide ameachia kibao anachokiita jina la "Chief", akimshirikisha malkia wa Afrobeats kutoka Nigeria, Tiwa Savage na sasa kinashika kasi kila kukicha.
Wimbo huo wa Koffi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na ambaye jina lake halisi ni Antoine Christophe Agbepa Mumba, ni tofauti na nyimbo nyingine za miondoko yake ya soukous ambayo imemjengea jina kubwa barani Afrika.
"Chief" umetoka na video inayomuonyesha mfalme huyo wa Soukous ambaye pia anajulikana kwa ustadi wa kutunga na kutayarisha nyimbo, akiimba pamoja na Tiwa pamoja na madansa wa kike waliovalia nguo za ufukweni wakinyonganyonga miili yao.
Kofi anaonekana kwa nyakati tofauti akiwa amevalia sare za jeshi na katika maeneo mengine nguo tofauti za kiraia.
Video hiyo imehaririwa na Clarence Peters.
Mpango huo haukuripotiwa awali kutokana na wawili hao kufanya siri, lakini matokeo yake yanaonekana kuwakamata mashabiki wa muziki na tayari hadi leo asubuhi video hivyo ilikuwa ishaangaliwa mara milioni 1.3 baada ya kuwekwa You Tube.
Mmoja wa wafuatiliaji You Tube anayejiita Fidel amefurahishwa na kazi hiyo akiandika "wote hao ni moto. Jamani wote mnafanya vizuri".
Mwingine anayeitwa Gesmson ameandika chini ya video hiyo akisema "Koffie hajawahi kutukera", huku mwingine, anayejiita Simon lkegbunem akisema "Tiwa, wewe ni kipenzi. Kolabo ya aina yake".
Shabiki mwingine anayeitwa, Rony Mudib ameandika "Koffi, kadiri anavyozeeka anaingia zaidi na zaidi katika malegendi, anaingia kila aina ya muziki, yeye ni GOAT (great of all time) wa kweli".
Kofi, ambaye pia hujiita Mopao, ametamba kwa vipindi tofauti na nyombo tofauti zilizoteka hisia za Waafrika kama "Loi", "Generation Bercy", "Papa Bonheur", "Andrada" na "Selfie" ambao bado unatamba.
Savage aliibukia London ambako alikuwa mwimbaji muitikiaji wa wanamuziki nyota kama Mary J.Blige na George Michael kabla ya kurudi Nigeria ambako ametajwa kuwania na kushinda tuzo kadhaa baada ya kutoa albamu yake ya kwanza ya EP inayoitwa Sugarcane.
Mwaka 2004, mkali huyo wa "Love in Yellow" alishirikiana na Mi Casa, Lola Rae, Sarkodie, Diamond Platnumz na Davido katika wimbo wa "Africa Rising".