Watu wenye silaha wamevamia kijiji kimoja cha kaskazini mwa Nigeria na kuua Waislamu 16 waliokuwa wanasali ndani ya Msikiti na kuteka nyara watu wengine wengi.
Mkuu wa serikali ya kijiji hicho cha Ba'are katika eneo la Mashegu kwenye jimbo la Niger la kaskazini mwa Nigeria, Bw. Alhassan Isah Mazakuka amesema kwamba uvamizi na ukatili huo wa kutisha ulifanyika nyakati za alfajiri ya kuamkia jana Ijumaa wakati Waislamu wakiwa wamo ndani ya Msikiti wanasali.
Amesema makumi ya watu wenye silaha walifika kijijini hapo wakiwa na pikipiki na kuanza kushambulia watu na kuiba. Waliingia Msikitini na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa katikati ya Sala na baadaye kuiba na kutoweka.
Shambulio hilo ni la karibuni kabisa kufanyika katika maeneo ya kaskazini magharibi na kaskazini-kati mwa Nigeria ambako watu wenye silaha wamekuwa wakishambulia maeneo ya ndani, kufanya mauaji ya kiholela na kuteka watu kwa ajili ya kuomba fidia.
Mazakuka ameliambia shirika la habari la Associated Press kwa njia ya simu jana Ijumaa kwamba, wavamizi hao ni watu hatari sana. Wameua Waislamu 16 waliokuwa ndani ya Sala na kuteka watu wengine wengi sana. Hatujui ni watu wangapi wametekwa nyara kwani idadi yao haihesabiki.
"Tuna tatizo kubwa la majambazi hapa kijijini petu," ameendelea kulalamika Mazakuka na kuongeza kuwa, tunachoomba ni dua zenu tu. Magenge yanayofanya ukatili huo si binadamu. Utawavamia vipi watu wanaofanya ibada Msikitini na kuwaua kwa umati kama hivyo? Serikali inatusaidia lakini bado tunahitaji mno kusaidiwa.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii
Follow Us
Subscribe