Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia watoto, UNICEF limesema kuwa maelfu ya watoto wameyakimbia makaazi yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako jeshi la taifa linapambana na waasi wa M23.
Taarifa mpya ya shirika hilo imeeleza kuwa tangu mwezi Machi mwaka huu, watu zaidi ya 190,000 walilazimika kuvipa kisogo vijiji vyao katika wilaya za Rutshuru na Nyiragongo, ikiongeza kuwa nusu ya idadi hiyo ni watoto.
''Maelfu ya watoto wanakabiliwa na kitisho na hawawezi kupata huduma za msingi ambazo ni muhimu kuwanusuru katika mzozo huu,'' amesema Grant Leaity, Mkurugenzi Mkazi wa UNICEF katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), baada ya kufanya ziara katika wilaya ya Rutshuru jana Jumamosi. Wilaya hiyo iko katika Jimbo la Kivu Kaskazini.
Suluhisho bado liko mbali
Leaity aliongeza kuwa yamkini watoto wataendelea kukabiliwa na masaibu hayo, kwa sababu bado watu wana hofu kurejea katika vijiji vyao.