Nandy alia ubaguzi tuzo za Afrima, Serikali yaombwa kuingilia kati

Katika hali isiyotarajiwa, mwimbaji wa Bongofleva, Nandy amedai yeye na mwenzake  Zuchu walipata mapokezi na uangalizi mbovu kutoka kwa waandaji wa tuzo za All African Music Awards (Afrima) nchini Nigeria.

Nandy na Zuchu wakiwa ni wasanii pekee kutoka Tanzania waliohudhuria hafla ya utolewaji wa tuzo hizo, walikuwa wanawania kipengele cha msanii bora wa kike Afrika Mashariki ambacho ushindi ulikwenda kwa Nikita Kering wa Kenya

Akizungunza na wanahabari, Nandy amesema ubaguzi ulionekana hasa wakati wa kufanya  mazoezi ya kujiandaa kutumbuiza na kuiomba Serikali kuandaa tuzo kwa ajili ya wasanii wa muziki nchini.

“Tunalalamika, haukuwa wakati sahihi wa kusema wakati ule tunarudi, mtasema kwa sababu tumekosa tuzo, sio kwamba hatustahili kushinda, Zuchu anastahili tuzo, mimi ninastahili tuzo, kila mtu anastahili, pia hatupingi kwa ile tuzo waliyompatia binti wa Kenya,” amesema. 

"Lakini kuna ile treatment mtu kuona angalau sijapata tuzo, sijapoteza muda kuna hiki, treatment ambayo nimepata kwa hawa watu ni nzuri ambayo next time nitafikiria kwenda tena, lakini treatment haikuwa nzuri kila mmoja analalamika kivyake. Mara kina Zuchu wamefika hamna sehemu ya kulala, wamekwenda kulala sehemu nyingine" amesema Nandy.

Nandy amesema yeye alishindwa kutumbuiza kutokana waandaaji hawakumpa vitu alivyohitaji  hata Zuchu ambaye alitumbuiza alikumbana na mengi ya kibaguzi.

"Kuepusha maneno ni mara mia nionekana sijatumbuiza, ni bora niache kuliko fedhea, Zuchu alitumbuiza vizuri japo kuna watu wawilli watatu wanaongea hivi na vile maana hawajua alichopitia" amesema Nandy na kuongeza;

"Zuchu alikuwa kwenye mazoezi, akaja msanii mkubwa wa Nigeria, akaambiwa muda umeisha, lakini menejimenti yake ipo wazi ikawaambia huyu atamaliza ndio aingie huyo. Ukitoka hapo unajihisi  nimeonekanaje, yaani mimi sistahili kufanya mazoezi yangu nikamaliza yakawa mazuri, tujadili tufanye nini tuache kushoboka na haya mambo ya Nigeria," amesema Nandy.

Kufuatia hilo, Nandy ameiomba Serikali kuwaleta wasanii tuzo za nyumbani ili kuacha kile alichoita kushobokea tuzo za Nigeria, pia mashabiki nchini wanapenda kuona wasanii wao wakishinda tuzo.

"Serikali hili suala waliangalie, na pia kama kuna wadau wanaweza kuleta hivi tuzo wazilete, mimi mwenyewe nilikuwa nimekaa kwenye ndege nawaza, kama nimeweza kufanya Nandy Festival kwa nini nisitengeneza tuzo, ni connection na sponsorship" amesema na kuendelea;

"Jamani nina tuzo zangu zimesajiliwa Basata, halafu kwenye hizi tuzo nataka Wizkid aje kutumbuiza nchini kwetu, nataka Burna Boy, Diamond, Zuchu watumbuize nahitaji kiasi hiki ili tufanikishe hili, wapo ambao watatoa," amesema Nandy.

Hivi karibuni mtayarisha mkongwe wa muziki Bongo, Master Jay aliliambia gazeti hili kuwa tuzo nyingi za kimataifa hasa kutoka Afrika hazina mchango wowote wa kuikuza Bongofleva kwa kile alichodai ni mradi wa watu wachache kujinufaisha. 

"Haziongezi mauzo, zinasaidia nini? labda BET, ila hizi nyingine ambazo zinatengenezwa na watu wa Afrika kwa sisi ambao tunajua kiundani, ni ujanja ujanja tu," alisema  Master Jay.

Ikumbukwe mwaka jana Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ilithibitisha kuwa mwaka huu kutakuwepo na tuzo za muziki baada ya kukosekana kwa kipindi kirefu. Serikali aliwahimiza wadau wote wa sekta hizo kukaa mkao wa kula kwani itaandaliwa kamati ya kuratibu suala hilo na vitawekwa vigezo na masharti ili kuwa na uwazi na ukweli kwenye utoaji wa tuzo hizo.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii