Harmonize azidi kupamba moto kwenye ulimwengu wa muziki

WALISEMA muziki ni vita kutokana na kila msanii kujipambania kutoboa na kujitangaza ndani na nje ya Afrika.

Harmonize alitoa ya moyoni vita na vikwazo ambavyo anapitia kwenye muziki wake, lakini bado anaendelea kupambana mpaka sasa.

Harmonize yupo kwenye kibarua kigumu ambacho wengi wanamuangalia kwa umakini kuona kama atatoboa au ataishia njiani kama baadhi ya wasanii ilivyokuwa miaka ya nyuma. Hawa hapa ni wasanii ambao walikuwa chini ya usimamizi wa mameneja wenye majina makubwa na kutamba, lakini walipoondoka mikononi mwao tu basi wamepotea.


Z-ANTO

Msanii huyu hakuna ambaye alikuwa hamjui wakati akiwa katika kundi la Tip Top Connection baada ya kutamba na ngoma kali ya ‘Mpenzi jini’.

Z-Anto baada ya ngoma hiyo alikuja na ngoma ya Mpenzi kiziwi ambayo nayo ilibamba kutokana na mashairi yake.

Baada ya nyimbo hizo alianza kupotea taratibu na mwisho wa siku akapotea kabisa kwenye muziki na hata alipojaribu kurudi hajawa kama alivyokuwa zamani. Kwa sasa ni msanii wa kawaida tofauti na miaka iliyopita.


SPACK

Msanii huyu naye miaka ya nyuma akiwa chini ya Tip Top Connection alitamba na ngoma ya Usiniache ambayo alimshirikisha Chid Benz akiwa wa moto.

Baadaye alikuja na ngoma ya Nipe ripoti akiwa na Madee zote zikienda mtaani na kutesa mitaani.

Lakini baada ya ngoma hizo na kuondoka Tip Top Connection amepotea na mwaka huu amerejea akiachia ngoma ya Haiko sawa lakini ni kama vile hajaachia nyimbo yoyote ile.


MB DOG

Miaka ya nyuma ilikuwa ukianza kutaja majina ya wasanii wanaojua kutunga mashairi ya mapenzi usingeacha kutaja jina hili.

Akiwa na Tip Top Connection alitamba na ngoma za Ina Maana, Mapenzi kitu gani, Natamani na Latifa zilizofanya vizuri na kutamba kila kona.

Baada ya kutoka Tip Top alikaa kimya kwa muda kisha akarudi na kuachia ngoma ya Sagaplasha akimshirikisha Madee. Wimbo huo ulikuwa mkali lakini haukusogea kama ambavyo nyimbo zingine zilivyokuwa.

Hadi sasa MD Dog yupo nyumbani akiendelea na maisha mengine nje ya muziki.


RICH MAVOKO

Mavoko aliingia Wasafi akiwa ametoka kuachia ngoma ya Pacha wangu akiwa na katika kundi hilo alifanya nyimbo ya Mpe Habari, Rudi na Sherii.

Baada ya kutoka kila alichoachia hakijabamba sana kama zamani.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii