MWAKA 2021 huo unakaribia kwisha. zimebaki siku 18 kuuambia kwaheri.
Wakati watu wataukumbuka kwa mambo mbalimbali yakiwemo ya kuhuzunisha na ya kufurahisha huenda kwa msanii wa Bongofleva, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ ukawa mwaka alioupiga mwingi. Hii ni kutokana na kufanikiwa katika mambo mbalimbali yakiwemo ya muziki, biashara na mahusiano.
KUFUNGUA LEBO
Msanii huyo alianza vizuri pale mwezi Machi alipotambulisha lebo yake. Lebo hiyo aliyoipa jina la Next Level Music tayari ameanza kurekodi nyimbo zake ikiwemo remix ya wimbo wa Jenifer alioimba na msanii wa Nigeria, Guchi. Pia lebo hiyo ikiwa na miezi michache imemsaini msanii mmoja na kuonyesha kufanya vizuri kwenye mitandao mbalimbali ya kuuza muziki.
Msanii huyo sio mwingine bali ni Macvoice ambaye kwa sasa na bosi wake wanatesa na wimbo wa ‘Tamu’ huku mwenyewe kibao cha kwanza kilichomtambulisha sokoni kikiwa ni ‘Nenda’ alichoachia Septemba, mwaka huu na wiki moja iliyopita ameachia wimbo wa ‘Mama mwenye nyumba’.
Hata hivyo, Rayvanny anamiliki lebo hiyo, huku akiwa bado yupo lebo ya Wasafi na hivyo kula huku na kule.
KUTUMBUIZA MTV EMMA
Mwaka huu Rayvanny alijua kuipeperusha bendera ya Tanzania vyema baada ya kuwa msanii kutoka Bara la Afrika kutumbuiza katika tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV EMA) 2021.
Tuzo hizo zilifanyika Novemba 14, mwaka huu nchini Hungary katika Ukumbi wa Budapest Spotarena. Katika usiku wa tuzo hizo wasanii mbalimbali walihudhuria na wengine kutwaa tuzo akiwemo Ed Shereen, Nicki Minaj, Rapa Lil Nas na wengine wengi.
Rayvanny alipanda katika jukwaa la tuzo hizo kuimba wimbo wa ‘Matetema’ alioshirikishwa na msanii Maluma ambaye alishinda kipengele cha mtumbuizaji bora kutoka nchi ya Latin America.
CHATI ZA BILLBOARD
Ikiwa zimepita wiki mbili tangu aonyeshe makeke kwenye tuzo hizo kubwa za MTV EMA, Rayvanny kapata baraka nyingine kuwa Mtanzania wa kwanza na msanii kutoka nchi za Afrika Mashariki kuingia kwenye orodha ya miziki inayofanya vizuri duniani ‘Billboard Chat’.
Huko Rayvanny anabebwa na wimbo wa ‘Matetema’, hali inayoonyesha ishara nzuri katika kushirikiana na wasanii wakubwa ambao wanapata tuzo za kimataifa.
KUFUNGUA MGAHAWA
Septemba, mwaka huu aliweka wazi kufungua mgahawa wake alioupa jina la Havanna uliopo maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Tayari mgahawa huo umeanza kufanya kazi na kupitia Instagram yake aliweka video kuonyesha huduma mbalimbali zinazopatikana hapo na kutumia nafasi hiyo kuwakaribisha watu kumuunga.
Kwa kufanya hivyo, Rayvanny anaongeza idadi ya wasanii wa Bongo ambao wameamua kuwekeza katika biashara ya chakula akitanguliwa na dada zake - Shilole na Eshe Buheti.
MAHUSIANO NA PAULA
Msanii huyu katambaa katika uhusiano na Paula na ni moja ya jambo kubwa kwa msanii huyo ukizingatia kulikuwa na panda shuka katika mahusiano yao hadi kufika hatua ya kupelekana polisi baada ya kuania picha akiwa na mrembo huyo ambaye ni mtoto wa msanii wa Bongofleva Kajala Masanja.
Baada ya sakata lao kumalizika kifamilia, Rayvanny akaona isiwe siri tena na kuamua kuweka mambo hadharani na Paula kabla ya kwenda masomoni nchini Uturuki. Paula alijua kuwanyoosha watu kwa ‘mapichapicha’ mitandaoni kila uchao wakiwa na msanii huyo.
Licha ya Rayvanny kutowahi kuzungumzia mahusiano hayo, lakini kwa kumuona tu unaona wazi kuwa anayafurahia, huku mama mkwe wake Kajala akionekana kuyaunga mkono na kumuita ‘son’ hasa pale anapoandika ‘comment’ za kumpongeza anapofanya jambo fulani zuri. Pia Julai mwaka huu Kajala alimkaribisha msanii huyo katika sherehe ya kuzaliwa kwa Paula, wakacheza muziki mbele yake na kulishana keki. Hii yote inaonyesha amepata baraka kwa mkwewe.