HALIMA KOPWE MISS TANZANIA , RAIS SAMIA KUJENGA UKUMBI WA KIMATAIFA JIJINI DAR


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Mhe. Rais Samia imedhamiria kuinua kuinua kiwango cha mashindano ya urembo nchini  ikiwa ni pamoja na kujenga ukumbi wa kimataifa  katika jiji la Dar es Salaam.



Akizungumza usiku wa kuamkia leo Mei 21, 2022 kwenye kilele cha mashindano ya kumtafuta  Miss Tanzania 2022 ambapo Halima Kopwe toka Mtwara ametwaa taji hilo, Mhe . Mchengerwa amesema ukumbi huo  licha ya kufanyiwa kazi mbalimbali za Sanaa na burudani pia utatumika kwenye mashindano ya kimataifa ikiwa ni pamoja na shindano la Miss Tanzania.

 "Ukumbi huo unatarajiwa kuongoza kwa ubora na ukubwa barani Afrika ambapo utachukua takribani watu elfu ishirini" amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuwashika mkono washindi wote na kufafanua kuwa washiriki wote walioshiriki shindano hili hadi kufika fainali ni washindi.

Amewapongeza waandaji wa shindano hilo kwa uratibu mzuri  ambapo ameongeza kuwa washiriki  wamefanya kazi nzuri ya ubunifu na Sanaa.

Pia amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ndiyo Wizara pekee inayowapa furaha na faraja watanzania wengi.

Pia Mhe. Mchengerwa amesema Filamu ya Royal Tour imesaidia kufungua milango na kuitangaza Tanzania  duniani na kuwataka wasanii kutumia fursa hiyo kutengeneza ajira na vipato.

Miss Tanzania kwa mwaka huu; Halima Kopwe amejishindia gari  dogo aina ya Benzi lenye thamani ya shilingi milioni 30 na  fedha taslimu shilingi milioni kumi.


Shindano hilo limefanyika jijini Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Mlimani City na kuhudhuriwa na mamia ya washabiki wa urembo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii