Ilikuwa Kuelekea mwishoni mwa 2019 Harmonize aliamua kuondoka kwenye lebo ya WCB ya Diamond Platnumz akiwa ni msanii wa pili kufanya hivyo baada ya Rich Mavoko ambaye alidumu hapo toka Machi 2016 hadi Julai 2018.
Harmonize aliondoka WCB akiwa tayari ametoa Extended Playlist (EP) moja, Afro Bongo akiwashirikisha Yemi Alade, Mr. Eazi na Burna Boy wote toka Nigeria, pamoja kushinda tuzo moja ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2016.
Hata hivyo, kuondoka WCB haikuwa kazi rahisi, kwa mujibu wa Harmonize mwenyewe alidai kuwa ili kuvunja mkataba wake wa miaka 10 na lebo hiyo, ilimlazimu kulipa Sh600 milioni.
Usiku wa uzinduzi wa albamu yake ya Afro East, Machi 14, 2020 aliulizwa na Mtangazaji Diva kama tayari amelipa fedha hizo. Jibu la Harmonize lilikuwa ameshamaliza deni hilo ambalo awali alidai lilipelekea kuuza nyumba zake tatu.
Akiwa kwenye jukwaa la Wasafi Festival mwaka 2019, Diamond alieleza kwa hisia kali kusalitiwa na mtu wake wa karibuni aitwaye Jeshi. Huyu alikuwa ni Harmonize ambaye kwa wakati huo ndio tetesi za yeye kujitoa WCB zilikuwa zimeshika kasi kwenye mitandao na kwingineko.
Mara baada ya kusaini WCB mwaka 2015, Harmonize alitoa wimbo wake wa kwanza ‘Aiyola’ chini ya lebo hiyo ukiwa umetayarishwa ndani studio za Kazi Kwanza Records na Prodyuza Maxmaizer.
Wakasafiri hadi Jijini Johannesburg, Afrika Kusini kufanya video ya wimbo huo na Director Nick Roux, Diamond hakuona tabu kutoa fedha kwa ajili ya kufanya video hiyo inayotajwa kuwa ya gharama kubwa kwa msanii anayechipukia.
Kwa mujibu wa Diamond, video ya Aiyola iligharimu Sh39 milioni, kisha ikafuata video za ngoma ‘Bado’ waliyoshirikiana ambayo pia ilifanyika Afrika Kusini, hii iligharimu Sh51 milioni. Hivyo, video mbili za Harmonize akiwa bado msanii mchanga katika muziki, ziligharimu Sh90 milioni.
Hata hivyo, kabla ya Aiyola kutoka tayari Harmonize alikuwa amesharekodi wimbo uitwao Kidonda Changu ambao hakufanya vizuri, ni kipindi kabla hajasaini WCB. Wimbo huo ndio ulipelekea Diamond kuona Harmonize ana kipaji kikubwa ambacho hakijapa usimamizi.
Alichofanya Harmonize ni kumtumia Diamond wimbo huo kupitia WhatsApp na akaupenda, ndipo akampatia namba za Meneja, Ricard Momo kwa ajili ya mawasiliano.
Kwa mara ya kwanza wakakutana katika ukumbi wa Dar Live, Dar es Salaam ambapo Diamond alikuwa na shoo yake, basi Harmonize akapatiwa nafasi ya kutumbuiza wimbo wake huo, Kidonda Changu. Na tangu hapo mengine yakabaki kuwa historia.
Wakati Hamonize anatoka mkoani kwao, Mtwara kwenda Dar es Salaam kwa mara ya kwanza kwa lengo la kuonana na Diamond, aliibiwa simu kitu kilichofanya akaghairishi safari hiyo na kurudi nyumbani na kujipanga upya.
Juni 17, 2018 Harmonize alikuwa na shoo ‘Kusi Night’ Dar Live, Diamond ambaye hakutangazwa kuwepo kwenye shoo hiyo, alikuja kama ‘suprise’, ujio wa Diamond ulimtoa Harmonize machozi kutokana ni hapo walikutana kwa mara ya kwanza.
Katika shoo hiyo wawili hao walitumbuiza nyimbo mbili walizofanya pamoja ambazo ni Bado na Kwangwaru ambayo ndio ilikuwa kwenye kilele cha mafanikio yake.
Kwa mujibu wa Harmonize, awali alipanga kumshirikisha msanii Davido kutokea Nigeria katika wimbo huo lakini baadaye akabadili uamuzi wake na kumshirikisha Diamond. Harmonize alianza kurekodi wimbo huo akiwa nchini Nigeria huku akimsubiria Davido ambaye alikuwa nchini Marekani.
Mwaka mmoja baadaye, Harmonize akaondoka katika lebo hiyo, mgogoro wa kimaslai na kile alichoita kunyanyapaliwa, ndivyo vilipelekea kuchukua maamuzi hayo.
Mkataba wao ilikuwa ni kwamba kila ambacho Harmonize ataingiza kupitia muziki, basi Diamond (WCB Wasafi) atachukua asilimia 60 na Harmonize asilimia 40. Ukiwa mkataba huo wa miaka 10 ulisaniwa rasmi mwaka 2015, basi ungemalizika mwaka 2025, hivyo Harmonize alitumikia takribani miaka minne tu ya mkataba huo.
Oktoba 24, 2019 Harmonize akihojiwa na kipindi cha XXL cha Clouds FM, alidai kuwa ili kuvunja mkataba wake na WCB ilimlazimu kulipa Sh500 milioni ila baadaye zikaongezeka Sh100 milioni, kutokana hakuwa na fedha hizo ilimlazimu kuuza hizo nyumba zake tatu.
“Kiukweli sikuwa na fedha, nikauza baadhi ya mali zangu, kuna sehemu nilikuwa na nyumba kama tatu ilinibidi niuze, tukalipa, î alisema Harmonize. Novemba 19, 2021 Harmonize akizungumza na Wanahabari Uwanja wa Ndege Dar es Salaam (JKIA) alidai licha ya kulipa fedha hizo, WCB hawakumpatia hati ya kuvunja mkataba, baada kuzungushwa sana aliamua kumtumia Hayati Rais John Magufuli.
“Nikaamua kumpigia simu Rais Magufuli nikamuelezea kile kinachoendelea na namshukuru sana, kwani aliagiza nipewe hati ya kuvunja mkataba. Nakumbuka siku hiyo Diamond alikuwa anasafiri kwenda ziarani Marekani, wakatakiwa wasiondoke bila kunipa hati” alisema Harmonize.
Baada ya kuachana na WCB, Harmonize aliachia albamu yake ya kwanza, Afro East ambayo ilizinduliwa Machi 14, 2020 na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jayaka Kikwete.
Albamu ya Afro East ambayo ina nyimbo 18 aliwashirikisha wasanii kama Burna Boy, Mr. Blue, Lady Jaydee, Morgan Heritage, Phyno, Skales, Yemi Alade, Mr. Eazi, Falz na Khaligraph Jones.
Haikuchukua muda, Harmonize akaanzisha lebo yake, Konde Music Worldwide huku Ibraah akiwa msanii wa kwanza kusainiwa ambaye Mei 8, 2020 aliachia EP yake, Steps ikiwa na nyimbo tano. Hadi sasa lebo hiyo ina wasanii wengine kama Angella, Country Boy, Young Skales toka Nigeria, na Cheed na Killy waliojiunga hapo baada ya kuondoka Kings Music yake Alikiba.