Kutoka kuwa mshiriki na kuzindua filamu ya Tanzania: The Royal Tour, kufanya mazungumzo na ikulu ya White House hadi kuanza kujenga daraja kati ya kampuni za filamu za Marekani na wacheza filamu wa Tanzania.
Ndivyo Rais Samia Suluhu Hassan anavyofanya kazi hivi sasa nchini Marekani ambako alikwenda wiki iliyopita, pamoja na mambo mengine kuzindua filamu hiyo iliyoongozwa na mwandishi maarufu wa Marekani, Peter Greenberg, hafla iliyofanyika jana Jumatatu usiku.
Baada ya filamu hiyo kuonyeshwa katika ukumbi wa jumba la makumbusho la Guggenheim jijini New York, Rais Samia alipata wasaa wa mazungumzo na Greeberg na baadaye kupokea maswali na maoni kutoka kwa waalikwa.
Mmoja wa waliouliza maswali alikuwa msichana aliyejitambulisha kwa jina la Maria.
"Kwa muigizaji mdogo wa kike ambaye najivunia sana nchi yangu, ni ushauri gani au ni kitu gani serikali yangu itatoa kuendeleza kile ulichoanzisha, ambacho ni kizuri, kuendeleza kuionyesha nchi yangu, kuendeleza kufuata nyayo zako kuionyesha dunia ni kwa namna gani Tanzania ni sehemu nzuri," ameuliza Maria.
"Kwa kweli nimeanza kuunganisha waigizaji wa Tanzania na dunia," amesema Samia.
"Jana nilikuwa na mkutano mzuri na taasisi tano kubwa katika sekta ya usafiri hapa Marekani, kwa hiyo nilikuwa na mazungumzo mazuri nao. Na moja katika mazungumzo hayo, nilikutana na mtu ambaye anafanya kazi Paramount na IMC. Kwa hiyo tulikuwa na mazungumzo mazuri na kuunganisha utamaduni na sanaa ya Tanzania katika sekta hiyo.
“Hivyo nadhani nimeanza kuwafanyia kazi. Nipe muda."
Paramount Pictures ni kampuni kubwa ya filamu ya Marekani ambayo pia inafanya kazi ya usambazaji wa kazi hizo za sanaa na ni sehemu ya kampuni kubwa duniani ya Paramount Global.
Ni moja ya kampuni kubwa tano za filamu duniani, ikishika nafasi ya tano kwa ukongwe ikiwa nyuma ya Gaumont Film ya Ufaransa iliyoanzishwa mwaka 1895, Pathé (1896), Titanus (1904), Nordisk Film (1906), na Universal Studios (1912).
IMC Cinemas ni kampuni kubwa ya filamu ya Ireland ambayo ina majumba ya sinema nchini kote Ireland na Ireland ya Kaskazini. Ilikuwa sehemu ya kampuni kubwa ya Ward Anderson hadi mwaka 2013.
Baada ya jibu la Rais Sami, Greenberg, ambaye alifuraia kusikia Big Five katika nyanja nyingine baada ya ile ya wanyama iliyomo katika filamu ya Royal Tour, alisema leo watakuwa na mazungumzo zaidi yatakayohusu pia suala hilo la sanaa ya filamu.