Wapiga kura nchini Hungary leo wanapiga kura huku wakikabiliwa na kibarua kizito cha kuchagua muungano wa vyama vya upinzani wenye sura ya kimagharibi, au kuendeleza utawala wa waziri mkuu mwenye siasa za kizalendo Viktor Orban kwa muhula wa nne mfululizo. Kinyang'anyiro cha leo kinatarajiwa kuwa na upinzani mkali tangu Orban aingie madarakani mwaka 2010. Vyama sita vya upinzani vimeweka kando tofauti za kiitakadi na kuungana, vikidhamiria kukiondoa madarakani chama cha Orban cha Fidesz. Kura za hivi karibuni za maoni zilionyesha ushindani mkali lakini zilikiweka mbele chama cha Fidesz kwa kura kidogo. Mgombea wa nafasi ya waziri mkuu kupitia muungano wa upinzani Peter Marki-Zay, ameahidi kukomesha kukithiri kwa rushwa serikalini na kuinua hali ya maisha kwa kuongeza fedha katika sekta ya afya na elimu.