Dira 2050: NEEC tunawajibika kuinua kipato cha Mtanzania kufikia dola 7,000

Bazara la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limepewa jukumu la kuimarisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi ili kuchochea ukuaji wa kipato na kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Katibu Mtendaji wa NEEC, Jabiri Makame, amesema taasisi hiyo ina wajibu wa ziada katika kipindi hiki ambacho Tanzania inatekeleza dira hiyo, ikiwemo kuweka mikakati itakayosaidia kufikisha wastani wa kipato cha Mtanzania katika Dola za Marekani 7,000 kwa mwaka ifikapo 2050.

Makame ameyasema hayo wakati wa makabidhiano rasmi ya ofisi yaliyofanyika mkoani Dodoma, yaliyoshuhudiwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Aurelia Kamuzora.

Amesema kwa mujibu wa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Prof. Aurelia Kamuzora. ina jukumu muhimu la kuhakikisha wananchi wanapata fursa na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya uchumi.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa jukumu hilo unahitaji mikakati inayowezesha wananchi kuongeza uzalishaji, kukuza biashara na kuinua kipato chao ili kuchangia kufikiwa kwa malengo ya taifa ya muda mrefu.

Kwa upande wake, Prof. Kamuzora amesema ukuaji wa uchumi unapaswa kujengwa katika maeneo manne muhimu ambayo ni uzalishaji, ulaji, uwekezaji na mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Amesema wananchi wanapaswa kuhamasishwa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini au zinazotokana na rasilimali za ndani, hatua itakayosaidia kuongeza soko la bidhaa za ndani na kuchochea shughuli za uzalishaji.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa ili Tanzania iweze kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kupata mapato zaidi.

Amesema kuimarisha maeneo hayo kutasaidia kukuza uchumi wa taifa na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii