Wamiliki wa boti za mbao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wametangaza mgomo mkuu wa urambazaji kuanzia Novemba 16 kupinga marufuku hiyo.
"Ni vigumu kupata boti ya chuma katika miezi miwili au mitatu," anasema mwakilishi wa taaluma hii, ambayo imekosolewa sana kufuatia ajali nyingi za boti kwenye mito mbalimali katika miaka ya hivi karibuni nchini DRC. "Vifo hivi vya watu vinahusiana zaidi na usumbufu", akidai "kwamba waziri (wa Uchukuzi) aongeze muda wa makataa kwa miaka miwili."
Boti za mbao zenye injini zimepigwa marufuku nchini DRC tangu Novemba 15, 2026, katika juhudi za kupambana na ajali mbaya za boti majini. Hatua hii inapingwa na wamiliki wa boti hizi za mbao, ambao wameanzisha mgomo mkuu kuanzia Novemba 16.
Chanzo cha vuguvugu hili ni kanuni mpya za sekta hiyo zilizowekwa na serikali. Katika taarifa yake, Chama cha Wamiliki wa Boti za Mbao za Kongo kinashutumu hatua hiyo iliyochukuliwa bila mashauriano, kikiona kuwa inaathiri vibaya shughuli zake pamoja na usambazaji wa bidhaa kwa wakazi wa kando ya mto.
Wamiliki wa vyombo vya usafiri wanadai kuondolewa kwa kanuni hii na kuanzishwa kwa mazungumzo na mamlaka. Wanataka hasa Rais Félix Tshisekedi kuingiliwa kati, kwa sababu huu ni mgomo unaotenganisha mji mkuu Kinshasa na vituo vyake vya usambazaji kutoka magharibi mwa nchi na kaskazini-masharikii.
"Kitakachotokea siku ya Jumatatu asubuhi ni kwamba katika bandari zote, hakuna boti yoyote ya mbao itakayopakua na wala kupakia mizigo, na hakuna chombo chochote kitakachosafiri kwenye njia za Mto Kongo hadi tutakapopata uamuzi wa pamoja na serikali," anaonya Jérémie Mwabikungu, msemaji wa wamiliki wa vyombo vya usafiri vya mbao nchini, akizungumza na mwandishi wetu Pascal Mulegwa. "Ni vigumu kufuata masharti ya serikali, kwa sababu muda tuliopewa ni mfupi. Ni vigumu kutengeneza chombo cha chuma ndani ya miezi miwili au mitatu."
Anaomba kuongezewa muda na serikali ya Kinshasa: "Tunachotaka ni kwamba waziri aongeze muda kwa makataa haya kwa miaka miwili, ili tuweze kujipanga. Tunakubaliana kabisa na hatua ya kukomesha safari za majini nyakati za usiku. Tunakubaliana pia na suala la kuwapatia abiria wetu makoti ya kuokoa maisha, wakiwemo na wafanyakazi wetu wa melini. "
Jérémie Mwabikungu anatetea taaluma yake: "Tunashutumiwa kwa kusababisha vifo hivi. Hata hivyo, vifo hivi vinahusiana zaidi na usumbufu. Kuna makamishna wa mito wanaowasumbua waendeshaji boti, kuna mabaharia (vikosi vya majini). Wamiliki wengi wa boti, ili kuepuka kukabiliana na hili wakati wa mchana, wanapendelea kusafiri usiku."