OIF yaahirisha uchaguzi wa katibu mkuu wake kwa mwaka mmoja

Shirika la Kimataifa la Nchi Zinazozungumza Kifaransa (OIF) limeahirisha uchaguzi wa Katibu Mkuu wake kwa muda wa mwaka mmoja. Uamuzi huo umefikiwa leo, Novemba 16, 2026, jijini Phnom Penh nchini Cambodia, kufuatia ukosefu wa mwafaka miongoni mwa nchi wanachama.

Baada ya mazungumzo makali na kampeni yenye mvutano, wanachama kamili wa OIF wameshindwa kukubaliana kuhusu mgombea. Uchaguzi wa kumchagua katibu mkuu ajaye umeahirishwa kwa mwaka mmoja, vyanzo kadhaa vimeiambia RFI.

Katibu Mkuu wa sasa, Louise Mushikiwabo kutoka Rwanda, ataendelea kushikilia wadhifa huo kwa mwaka mmoja zaidi hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika. Hata hivyo, imeelezwa kuwa hatagombea tena katika uchaguzi huo ujao.

Uchaguzi huo uligubikwa na mvutano mkali kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Rwanda. DRC ilipinga vikali muhula wa tatu wa Mushikiwabo kwa kuishutumu Rwanda kuunga mkono waasi wa M23, na ilitishia kujiondoa katika shirika hilo endapo angechaguliwa tena.

Mbali na Louise Mushikiwabo, wagombea wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo ni Juliana Lumumba (kutoka DRC), Waziri Mkuu wa zamani wa Romania Dacian CioloČ™, na waziri wa zamani wa Mauritania Coumba Ba.

Nchi wanachama 53 zilizo na haki kamili ya kupiga kura ziliamua kuepuka kupiga kura ya siri ambayo ingeweza kuligawa shirika, na badala yake zikachagua kuahirisha uchaguzi ili kutafuta mgombea atakayekubalika na pande zote, kama ilivyokuwa desturi tangu mwaka 1997.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii