Urusi yashambulia madaraja mawili makubwa Kyiv

Urusi imeshambulia madaraja mawili makubwa huko Kyiv, na Ukraine imeshambulia daraja la Crimea kwa usiku wa pili mfululizo. Mashambulizi haya yana umuhimu mkubwa wa kiishara) kwa sababu yanatokea siku mbili kabla ya mkutano nchini China kati ya wakuu wa nchi za Urusi, Marekani na China.

Siku nyingine ya mashambulizi ya anga kati ya Urusi na Ukraine. Siku ya Jumanne, Novemba 17, Urusi ilishambulia madaraja mawili makubwa huko Kyiv. Kwa upande wake, Ukraine imelenga daraja la Crimea kwa usiku wa pili mfululizo.

Rais wa Ukraine aliwaonya wakazi kuhusu shambulio linalowezekana la Urusi katika siku zijazo. Wakati wa usiku, Urusi ilishambulia madaraja mawili makubwa huko Kyiv, ambayo tayari yalikuwa yamelengwa katika wiki za hivi karibuni, lakini hayakuwahi kushambuliwa kwa wakati mmoja. Yalifungwa Jumanne na mamlaka za eneo hilo, ambazo zilitangaza kwenye mitandao ya kijamii. Mifumo muhimu ya miundombinu pia imeharibiwa, na usambazaji wa maji na joto umevurugika katika baadhi ya vitongoji.

"Nao, huko Urusi, lazima wajue kwamba kwa kila moja ya matendo yao mabaya, kutakuwa na jibu letu la haki," ameonya Volodymyr Zelensky.

Muda mfupi kabla ya mashambulizi ya Urusi, Ukraine ilitangaza kuwa imelenga daraja la Crimea kwa siku ya pili mfululizo — daraja linalounganisha Urusi na eneo hilo lililonyakuliwa mwaka 2014 na Moscow kwa mbwembwe kubwa, ambalo ni ishara kubwa ya kisiasa kwa Rais Putin.

"Adui ameshambulia tena daraja la Crimea", gavana wa Crimea aliyewekwa na Moscow, Sergei Aksionov, amesema katika ujumbe kwenye jukwaa la X, akiongeza kuwa usafiri umesitishwa baada ya shambulio hilo. Kwenye rasi hiyo, watu wawili wameuawa katika "shambulio lililofanywa na ndege isiyo na rubani ya adui katika wilaya ya Leninski", kulingana na Sergei Aksionov.

Urusi pia ilidungua ndege zisizo na rubani 1,441 za Ukraine usiku, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imetangaza. "Katika usiku uliopita, vikosi vya ulinzi wa anga vilidungua ndege zisizo na rubani 1,441 za Ukraine," wizara hiyo ilisema kwenye Telegram.

Mazungumzo ya kihistoria

Wimbi hili la mashambulizi lina ishara kubwa sana kwa sababu linatokea siku mbili kabla ya mkutano nchini China kati ya Vladimir Putin, Xi Jinping na Donald Trump. Rais Putin anatarajiwa kuwasili siku ya Alhamisi mjini Shenzhen, kusini-mashariki mwa China, ambako atakutana na marais wenzake wa Marekani na China, pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC). Huu utakuwa mkutano wa kwanza wa aina yake kati ya Bw. Putin, Donald Trump na Xi Jinping.

Wakuu hao watatu wa nchi watafanya "majadiliano ya kina kuhusu kuhifadhi amani ya dunia na kukuza utulivu wa kimkakati katika uhusiano kati ya mataifa makubwa, ambayo yatakuwa na umuhimu wa kihistoria," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning alisema siku ya Jumatatu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii