Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeitaka Serikali ya Kenya kuanzisha uchunguzi wa haraka kubaini alipo mwanaharakati Mtanzania, Twaha Mwaipaya, anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana nchini humo.
Mtandao huo pia umeitaka Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ubalozi wake nchini Kenya, kuongeza jitihada za kidiplomasia ili kuhakikisha Mwaipaya anapatikana akiwa salama.
Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 26, 2026, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema mtandao huo umesikitishwa na kutokuwepo kwa taarifa rasmi na kamili kutoka kwa vyombo vya usalama vya Kenya kuhusu tukio hilo.
Kwa mujibu wa Wakili huyo, Mwaipaya aliripotiwa kupotea Jumapili, Oktoba 25, 2026, baada ya watu wasiojulikana kudaiwa kumfuatilia hadi maeneo ya nje kidogo ya jiji la Nairobi, kuvamia gari na kuondoka naye kwenda kusikojulikana.
“THRDC hadi inapotoa taarifa hii haikuwa imepata taarifa rasmi zinazoweza kuthibitishwa kuhusu alipo Mwaipaya, huku Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya ukieleza kuwa unaendelea kufuatilia suala hilo,” amesema Wakili Olengurumwa.
Amesema kutokuwepo kwa taarifa za uhakika kunaongeza hofu kwa familia yake na jamii, hivyo kutaka mamlaka za Kenya kutoa taarifa sahihi kuhusu hatua zinazochukuliwa.
Aidha, THRDC imeitaka Serikali ya Tanzania kuwasiliana kwa karibu na mamlaka za Kenya na kuhakikisha familia ya Mwaipaya inapata taarifa za kuaminika kwa wakati kuhusu mwenendo wa ufuatiliaji.
Imependekeza umuhimu wa Serikali kutumia njia za kidiplomasia na kibalozi kumsaidia raia wake aliyeko nje ya nchi, kwa kuzingatia sheria za kitaifa na mikataba ya kimataifa.
Vilevile, wanaharakati na wanasiasa kuzingatia tahadhari za kiusalama, kuwa na mawasiliano ya dharura na kuripoti vitisho kupitia njia salama.