Shambulio la droni mjini Nyala nchini Sudan, lauwa watu 21

Shambulio la ndege zisizo na rubani katika soko huko Nyala, mji mkuu wa kikosi cha wanamgambo wa Rapid Support Forces RSF eneo la magharibi mwa Darfur nchini Sudan, limewaua watu 21 na kuwajeruhi wengine wasiopungua 40.

 Daktari katika Hospitali ya Nyala amethibitisha kwamba watu 21 wameuawa katika shambulio la bomu la Jumatatu usiku na zaidi ya wengine 40 walijeruhiwa, ingawa hakuweza kutambua ni wapiganaji wangapi walikuwa wa kikosi cha RSF.

Wakati haya yakiarifiwa, wapiganaji wa RSF wamefanya shambulizi la ndege isiyo na rubani leo Jumanne kwenye kituo cha umeme katika mji mkuu Khartoum. Droni za wanamgambo wa RSF zilikilenga kituo cha transfoma cha Al-Markhiyat na kuvuruga usambazaji wa umeme katika sehemu kubwa za majimbo ya Khartoum na Al-Jazira.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii