Mkutano wa Afrika - Urusi unafanyika jijini Moscow

Mkutano wa tatu, kati ya viongozi wa mataifa ya bara la Afrika na Urusi, unafanyika siku ya Jumatano na Alhamisi, jijini Moscow.

Urusi inaendelea kutafuta ushirikiano wa karibu na mataifa ya Afrika kwenye masuala mbalimbali ikiwemo biashara,kilimo, usalama miongoni mwa mambo mengine.

Kwa miaka mingi sasa, mataifa ya Afrika yamekuwa yakishirikiana zaidi na mataifa ya Magharibi, lakini Urusi tangu mwaka 2019 ilipoanza mikutano hii, imeongeza ushirikiano wake na Afrika, hasa kwenye masuala ya usalama.

Wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa 48, wanashiriki kwenye mkutano huu wa siku mbili ambao unamkutania rais Vladimir Putin na marais zaidi ya 20, akiongoza mkutano huo na rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.

Rais Putin, amekuwa akikosoa namna mataifa ya Magharibi yanavyoendeleza ukoloni mambo leo barani Afrika, hasa kwa mataifa yaliyokuwa koloni ya Ufaransa katika eneo la Sahel.

Mkutano huu wa tatu unafanyika pia wakati huu, maelfu ya Waafrika wakiripotiwa kuajiriwa katika jeshi la Urusi kwenda kupigana kwenye vita nchini Ukraine, suala ambalo linatarajiwa pia kujadiliwa kwenye mkutano huu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii