Serikali imeendelea kuwapa kipaumbele wanafunzi wenye ulemavu kwa kuhakikisha wanashirikiana na wanafunzi wengine katika kuimarisha uadilifu, uwajibikaji na usawa kupitia Klabu za Maadili zilizopo shuleni.
Akizungumza Oktoba 26, 2026, baada ya kutembelea Klabu ya Maadili ya Shule ya Msingi Itumbili, iliyopo Wilaya ya Magu na yenye huduma za elimu jumuishi na elimu maalum, Afisa Maadili kutoka Ofisi ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa, Samwel Daud Omary, amesema wanafunzi wenye ulemavu wamekuwa wakiongeza hamasa katika klabu hizo kutokana na bidii yao ya kujifunza na kuzingatia uadilifu bila kubaguliwa.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa wanafunzi katika shughuli za klabu huimarisha umoja na uwajibikaji, jambo linalochochea juhudi za Serikali kuendelea kuziunga mkono klabu hizo.
Kwa upande wake, Mwalimu Mlezi wa Klabu ya Maadili katika Shule ya Msingi Itumbili, Diana Tang'are, amesema uwepo wa klabu hiyo umesaidia kupunguza utoro kutokana na kuimarika kwa ushirikiano miongoni mwa wanafunzi.
Naye, Mwalimu wa Lugha za Alama katika shule hiyo, Stella Mzimbu, amewataka wazazi kuacha kuwaficha watoto wenye mahitaji maalumu, akisema wana uwezo wa kupata elimu na kuchangia maendeleo ya jamii.
Hata hivyo, Afisa Maadili huyo ametembelea shule saba kati ya nane za msingi zenye Klabu za Maadili katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza, ambazo ni Chief Hangaya, Bujora, Kisesa A, Kisesa B, Bukandwe, Kahangara na Itumbili.
Imeandikwa| Martin Mbilinyi