Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara limewakamata watuhumiwa 10 wanaodaiwa kuhusika na makosa ya mauaji yaliyotokea katika Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, katika kipindi cha kuanzia Oktoba 2025 hadi Oktoba 2026.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Oktoba 26, 2026, imeeleza kuwa watuhumiwa saba (7) tayari wamefikishwa mahakamani, huku wengine watatu (3) kesi zao zikiendelea kufanyiwa upelelezi.
Miongoni mwa watuhumiwa ambao kesi zao bado ziko kwenye hatua ya upelelezi ni Emmanuel Paul na Abdalah Mohamed, wanaotuhumiwa kwa mauaji ya Leonard, mkulima mkazi wa Mtaa wa Madukani. Mtuhumiwa mwingine ni Mohamed Juma, anayetuhumiwa kwa mauaji ya mfanyakazi wake aliyejulikana kwa jina la Mohamed Kipara, mkazi wa Mtaa wa Madukani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watuhumiwa ambao kesi zao zimefikishwa mahakamani ni Ambrose Matepeli, Mudi Saidi, Ester Rokoine, Juma Athuman, Revocatus Finias, Juma Sembua na Juma Elifasi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara limewataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kutoa malalamiko yasiyo na ukweli. Badala yake, wananchi wanahimizwa kutoa taarifa sahihi kuhusu matukio ya uhalifu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.