SMAUJATA YAWATAKA WAZAZI KUSIMAMIA MALEZI YA WATOTO

Katibu wa SMAUJATA Taifa, Idara ya Watu Wenye Ulemavu, Ester Sanga, amewataka wazazi kusimamia malezi ya watoto wao kikamilifu, ikiwemo kudhibiti matumizi ya simu kwa watoto pale ambapo hakuna sababu ya msingi, ili kuwasaidia kukua katika misingi ya maadili mema.

Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) imeendelea kuwa jukwaa la kuelimisha jamii kuhusu namna ya kukabiliana na kutokomeza vitendo vya ukatili. Akizungumzia suala hilo leo Octoba 25, 2026 Ester amesema kuwapa watoto simu bila sababu ya msingi kunaweza kuwaweka katika mazingira ya kujifunza mambo yasiyofaa.

“ Kama hakuna sababu ya msingi, unampa simu ya nini? Kupitia simu, watoto wanaweza kujifunza mambo yasiyofaa, ikiwemo mavazi yasiyo na staha, kutazama filamu za vita na picha za ngono. Wazazi wawe makini katika malezi,” amesema Ester.

Ester amesisitiza kuwa kila mwanajamii anapaswa kuwa sehemu ya juhudi za SMAUJATA katika kupinga ukatili kwa kuhakikisha anachukua hatua za kuzuia vitendo hivyo na kutoa taarifa vinapotokea.

“Kila mtu awe huru kumlinda mwenzake ili tupunguze ukatili na pia tujenge familia zenye umoja na ushirikiano,” amesema Ester.

Akizungumzia visababishi vya ukatili wa kijinsia, Ester amesema baadhi ya vitendo hivyo huanzia katika familia, pale ambapo watoto wanapewa majukumu yanayopaswa kutekelezwa na wazazi, ikiwemo kubeba wajibu mkubwa wa kutunza familia.

Amesema pia baadhi ya wazazi wenye watoto wenye ulemavu huwaficha na kuwanyima fursa ya kupata elimu, hali inayoweza kuwanyima haki na huduma zinazostahili.

“Wazazi wanapopata watoto wenye ulemavu na kuwaficha bila kuwapeleka shule, huo pia ni ukatili. Kwa sasa kuna usajili wa watoto wenye ulemavu, lakini wazazi wengi hawajitokezi kuwasajili watoto wao. Hali hiyo inaweza kuwafanya wakose haki ambazo Serikali imepanga kuwapatia,” amesema Ester.

Katika hatua nyingine, Ester ameitaka Serikali, taasisi za elimu na sekta binafsi kuongeza juhudi za kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, hatua inayoweza kusaidia kupunguza vitendo hivyo katika jamii.

Amesema ukatili huathiri umoja wa jamii, husababisha maumivu na unaweza kusababisha vifo, huku akihimiza wananchi kutumia vyombo vya habari na njia nyingine zinazofaa kutoa elimu na kuhakikisha taarifa za vitendo vya ukatili zinawasilishwa kwa mamlaka husika.

Imeandikwa| Martin Mbilinyi

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii